Faida za matumizi ya ganda la yai "egg shell"

Chanzo cha madini ya kalshamu (calcium)

Maganda ya mayai hasa yatokanayo na kuku wa kienyeji, ni chanzo muhimu cha madini ya kalshamu (calcium) yenye faida katika miili ya wanadamu na wanyama wengine kwa kuimarisha mifupa, meno na viungo vingine muhimu mwilini. Kwa matumizi ya mwanadamu, yaloweke maganda ya mayai kwenye juisi ya limao ama kwenye siki (vinegar) kisha chuja na kutumia juisi hiyo hasa kwenye kachumbari na mapishi mengine yanayotumia limao ama siki (vimiminika hivyo vya limao na siki husaidia kurahisisha ufyonzwaji wa madini tajwa mwilini).

Kipodozi/Bidhaa ya kujipodoa

Kwa kutumia njia iliyotajwa hapo juu, unaweza pia kutumia mabaki ya mchujo wa juisi kupaka kwenye ngozi 'scrub' kwa ajili ya kuifanya iwe laini, nyororo na ya kuvutia.

Dawa ya kuondoa mwasho na maumivu

Maganda ya mayai yanaweza kusaidia kuondoa mwasho na maumivu kwenye ngozi kwa kuyaponda na kisha kuyaloweka kwenye siki ya matofaa 'apple cider vinegar'. Zipo taarifa kuwa Wataalamu wanatafiti uwezekano wa kutumia ngozi laini iliyopo kwenye maganda ya mayai, kupunguza maumivu ya baridi yabisi (arthritis), yabisi kavu (rheumatism) na kuoza mifupa (osteoporosis).

Hurutubisha udongo

Maganda ya mayai yakipondwa na kiasi kuchanganywa na udongo huongeza virutubisho muhimu vinavyohitajika katika kukuza mimea. Vile vile husaidia udongo kushikamana na kupitisha maji taaratibu hivyo kuuacha na unyevu wa kutosha kukuza mimea.

Dawa dhidi ya wadudu

Maganda ya mayai yaliyovunjwa katika vipande vya wastani hutumika kama silaha ya kuzuia paka wasilale bustanini na kuharibu mazao.

Kusafishia sufuria

Maganda ya mayai yakipondwa vyema yanaweza kutumika kung'arisha sufuria na vyombo vya kupikia.