Haya! Kisa 'mapenzi': Wabunge wa Tanzania watuhumiwa kudundana Malaysia

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanadaiwa kupigana huko Malaysia baada ya kukutana hotelini, wakati wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), walipokuwa katika ziara ya kikazi nchini humo.

Tukio hilo lilitokea siku nne zilizopita baada ya mbunge wa kamati hiyo kutoka CCM kuvamiwa alipokuwa akipata kifungua kinywa kwenye hoteli aliyofikia na wenzake wawili mmoja wa CCM na mwingine wa CHADEMA. Majina ya wabunge hao watatu tunayahifadhi kwa sasa kwa sababu hatukuwapata kujibu tuhuma hizo.

Hata hivyo, mbunge wa CHADEMA ambaye siyo mjumbe wa PAC haikufahamika ilikuwaje akawamo katika ziara hiyo.

Habari zilizolifikia gazeti hili (Mwananchi) jana zinadai kuwa chanzo cha ugomvi huo masuala ya
uhusiano na kwamba mbunge aliyevamiwa alipigwa vibaya.

Chanzo cha mbunge huyo kupigwa kinaelezwa kuwa ni hatua yake ya kuweka ujumbe kwenye mtandao wa WhatsApp unaowaunganisha baadhi ya wabunge, akiwasuta wenzake hao wawili kwamba wamekuwa wakichochea kuvunjika kwa uhusiano wake na mbunge mwenzake.

Ujumbe huo unadaiwa kuambatana na uliotumwa na wabunge hao wawili kwa binti mmoja anayefanya kazi katika benki moja mjini Dodoma ambaye pia anatajwa kuwa na uhusiano na mbunge huyo mwanamume, wakimtaka asiachane naye kwa maelezo kwamba mwenzao huyo atatamba.

Binti huyo alikuwa ametuma ujumbe kwenye mtandao wa pamoja na wabunge hao wawili akieleza kwamba ameamua kuvunja uhusiano wake na mbunge (mwanamume) kwa maelezo kwamba asingependa kuingia kwenye mvutano wa kimapenzi.

Baada ya kutuma ujumbe huo wabunge hao wawili (wanaotuhumiwa kumshambulia mwenzao), wanadaiwa kumjibu wakimsisitiza kuendelea na uhusiano huo mawasiliano ambayo yalikuja kunaswa na mbunge aliyeshambuliwa.

Inaelezwa kwamba baada ya kunasa mawasiliano hayo, mbunge huyo alichukua ujumbe wa wabunge hao kama ulivyo na kuuweka kwenye mtandao unaowaunganisha wabunge wengi akiwasuta kwamba ni wanafiki na kwamba wamekuwa wakihaha usiku na mchana kuhakikisha ‘ndoa’ yake inavunjika.

Kutokana na kuumbuliwa huko, wabunge hao walimvamia mwenzao hotelini na kumpiga mbele ya wenzake. Gazeti hili lilimpigia simu mbunge anayedaiwa kumpiga mwenzake kwa kiasi kikubwa na baada ya kuelezwa tukio zima na kabla ya ufafanuzi, alikata simu bila kujibu chochote.

Kiongozi wa msafara huo Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alipopigiwa simu na mwandishi wetu hata kabla ya kuulizwa kuhusu ugomvi huo alisema: “Hakuna kilichotokea. Mimi ni mwandishi wa habari kama wewe, hakuna kilichotokea na hakukuwa na ugomvi wowote.”

Alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka mtindo wa wabunge kusingiziwa kuwa wamefanya jambo fulani, huku akisisitiza kuwa kama kulizuka ugomvi asingeweza kuficha chochote.

via gazeti Mwananchi