Katibu Mkuu Kiongozi akutana na ujumbe wa Chuo cha St Thomas, Marekani

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na ujumbe kutoka Chuo cha St. Thomas cha Marekani uliomtembelea Ikulu jijini Dar es salaam leo Julai 16, 2014  (picha: Ikulu)

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue jana tarehe 16 Julai, 2014 alikutana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Thomas cha Minnesota, Marekani wanaotembelea Tanzania kujifunza uzoefu wa Tanzania katika masuala ya kiuongozi na anuwai ya tamaduni. Wanafunzi hao ambao kwa idadi yao ni wanafunzi 14 wanaochukua Shahada za Uzamivu na Uzamivu katika masuala ya Uongozi wa Kimataifa pamoja na Wakufunzi wao wawili, Dkt. Jean Pierre Bongila na Dkt. Artika Tyner.

Mkutano huu ni mwendelezo wa mkutano kama huu ambao Katibu Mkuu Kiongozi aliufanya mwaka
jana na kundi jingine la wanafunzi kutoka Chuo hicho ambapo aliwapa uzoefu wa uongozi na anuwai ya tamaduni katika Tanzania, Afrika na katika medani za kimataifa.

Kwa kutambua umuhimu wa nasaha walizozipata wanafunzi wa mwaka jana, Chuo hicho kiliomba na kukubaliwa fursa nyingine ya kuonana na Katibu Mkuu Kiongozi. Ziara ya wanafunzi hao ilianzia Arusha tangu tarehe 12 Julai, 2014 na itamalizika tarehe 17 Julai, 2014.

Pamoja na kupata fursa ya kuonana na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Arusha, wanafunzi hao walipata pia muda wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Arusha na baadaye Zanzibar. Na matarajio ni kuwa wanafunzi hao watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania sehemu mbalimbali za dunia watakakokwenda kufanya kazi.

Kwa ujumla, wanafunzi wamepata fursa nzuri ya kuuliza maswali yaliyogusa maeneo yote yanayohusu uongozi, siasa, uchumi, elimu, afya na utamaduni ambayo yalipata ufafanuzi wa kutosha kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi.