Maandamano Dar kupinga mauaji Mashariki ya Kati

TAASISI ya Hawzat-Imam-Swadiq (A.S), iliyopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, imepanga kufanya maandamano kesho kupinga mauaji yanayoendelea Mashariki ya Kati dhidi ya Wapalestina.

Mkuu wa taasisi hiyo, Hemed Jalala, akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema wanapinga vikali mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina na kuamua kufanya maandamano yataanzia katika kituo cha daladala cha Ilala Boma hadi Kigogo uwanja wa Bibo kuanzia saa tatu asubuhi hadi sita mchana.
“Hadi sasa maelfu ya Wapalestina wamepoteza maisha, hivyo jamii na taifa kwa ujumla tunapaswa kushirikana na kuonyesha kuguswa na mauaji hayo, kwani waathirika ni
watu wa dini zote.
“Kutokana na mauaji yanayoendelea nchini humo, watu wanashindwa kwenda misikitini na makanisani kufanya ibada na hata kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.” 
Jalala alisema maandamano hayo yatahusisha watu wa dini zote na yana kibali kutoka Jeshi la Polisi na kuiomba jamii kujitokeza na kushirikiana kuonesha hali ya umoja kupinga mauaji hayo kwa kuwa kunyamazia tatizo hilo ni kufanya kosa kwani hakuna hata dini moja inaruhusu mauaji ya binadamu mwingine.

Msemaji wa Taasisi hiyo Profesa Abdul Shariff, amesema kuwa wameamua kupaza sauti zao kulaani baada ya kuona Jumuiya mbalimbali za Kimataifa ikiwa imenyamaza huku mamia ya watu wakizidi kupoteza maisha.

Amesema kuwa inasikitisha kuona hata vyombo vya habari hasa vya Magharibi havitoi nafasi kubwa kwa mauaji hayo ukilinganisha na mauaji yaliyotokea kwa kulipuliwa kwa ndege Malyasia.

Viongozi na Mabalozi wa nchi mbalimbali wamealikwa ili nao waweze kushiriki katika kupaza sauti zao pamoja na Watanzania kulaani vitendo vinavyofanywa na Israel vya kuua watu wasio na hatia.