Madaraka Nyerere: Tujisahihishe

Tujisahihishe

Watanzania tuna sifa ya kuwa waoga sana kuwasahihisha wenzetu wanapokosea. Naomba kuwa tofauti kwa leo. Na ni kwa nia nzuri tu.

Kombe la Dunia la FIFA limeisha hivi karibuni na nilisikia (kwenye redio na runinga) na kuona kwenye maandishi, haswa kwenye mitandao ya jamii, matumizi yasiyo sahihi ya majina ya baadhi ya timu zilizoshiriki kwenye mashindano hayo.

"Ujerumani" iliandikwa "Ujeruman." Na kwa Kiingereza badala ya kuandika "Germany", baadhi ya watu waliandika "German." Tatizo hili la matumizi ya lugha lisichukuliwe kuwa ni kwa lugha au
majina ya kigeni pekee. Jana nikiwa kwenye ndege nilisikia mfanyakazi wa ndani ya ndege akitutangazia abiria kuwa "tumetua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerele." Huyo ni Mtanzania anashindwa kutamka "Nyerere." Na haikuwa mara yangu ya kwanza kusikia "Nyerere" kuitwa Nyerele." Kama ungeondoa muktadha ungefikiri alikuwa anazungumzia nyenyere.

Lakini jambo la kushangaza zaidi ni kuwa baada ya kutamka hivyo alianza kuongea kwa Kiingereza kutoa taarifa hiyo hiyo kwa abiria tuliokuwa ndani ya ndege, lakini alipoongea kwa Kiingereza alitamka "Nyerere" kwa usahihi.

Hii mifano inaashiria matatizo mawili. Kwa mfano wa kwanza ni kutojuwa matumizi sahihi ya majina au lugha ("Germany" ni nchi; "German" ni Mjerumani) au kutojali kuwa makini tunatamkaje majina au maneno (huyo huyo aliyetamka "Nyerele" anatamka "Nyerere" baada ya sekunde chache).

Nawasilisha hoja.

Madaraka @ Muhunda blog