Mawio yaburuzwa kortini na AP Media and Consultant Limited

MKURUGENZI Mtendaji wa kampuni ya AP Media and Consultant Limited, Bw. Peter Keasi, amefungua shauri la madai dhidi ya Mhariri wa gazeti la kila wiki la Mawio na mwandishi wa gazeti hilo Jabir Idrissa, akidai malipo ya billioni mbili kama fidia kwa kumkashifu yeye pamoja na kampuni yake.

Kupitia kwa wakili Mhe. Alloyce Komba wa kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza, Keasi amefungua shauri hilo katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. Anadai kukashifiwa kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti hilo namba 0098 la kati ya juni 5-11, mwaka huu.

Taarifa hiyo ilikuwa na kichwa cha habari kinachoeleza kuwa, “CCM kutumia billion 3.4 kujitangaza,” ambayo iliandikwa na Idrissa, ikionyesha kuwa kazi hiyo ya kujitangaza kwa CCM amepewa Keasi kupitia kampuni yake ya AP Media and Consultant Limited.

Katika kesi hiyo, Keasi amenukuu kipande kimoja cha habari kilichochapishwa na gazeti hilo
kikionyesha kuwa “nimeshangaa kuona chama changu kikitumia zaidi ya bilioni tatu kujitangaza.. Hawa watu hawana huruma kabisa na wananchi maskini. Wanachojua wao ni kula hadi kuvimbiwa.”

Keasi anadai kuwa maneno kama hayo yalimaanisha kuwa yeye ni mwizi wa fedha za chama kilichoko madarakani na hajali maslahi ya watu wengine.

“Kwa maneno haya, walalamikiwa wamemkashifu na kumshushia hadhi mlalamikaji mbele ya jamii, ofisi yake na katika biashara zake,” sehemu ya hati ya madai inaeleza.

Inadaiwa kuwa walalamikiwa walichapisha taarifa hiyo bila kuzingatia miiko na weledi wa kazi yao wa kutoa taarifa zilizo za kweli, sahihi na zilinazozingatia usawa wa pande mbili za wahusika kwa vile hapakuwa na ukweli wowote kuwa mlalamikaji amepewa kazi hiyo na CCM.

“Walalamikiwa bila kuwa na uhalali na ukweli wowote walichapisha taarifa zinazoonyeha kuwa mlalamikaji ni mwandishi mwandamizi wa magazeti ya Daily News na Habari Leo yanayochapishwa na kampuni ya Tanzania Standard Newspapers,” hati ya madai inaeleza.

Keasi ameeleza kuwa ukweli ni kwamba aliajiliwa na kampuni hiyo mnamo Aprili 1, 1998 hadi Octoba 27, 2012, ambapo alijihuzuru mwenyewe na kujihuzuru kwake kulikubaliwa na uongozi wa kampuni ya TSN.

Katika taarifa hiyo, walalamikiwa walieleza pia kuwa mlalamikaji atajipatia millioni 500 kutoka CCM kwa kazi hiyo ya kijitangaza.
Hapo awali, mlalamikaji aliwaandikia walalamikiwa akitaka wamwombe radhi na kusahihisha taarifa hiyo kwenye toleo la gazeti litakalofuata na taarifa hiyo ichapishwa ukurasa wa kwanza na wa pili na yenye uzito sawasawa na ile iliyochapishwa awali, lakini wamekataa kutekeleza matakwa yake.