Mbunge atuhumiwa kumdunda baba yake sababu ni mlevi

MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses Machali, anatuhumiwa kumpiga baba yake mzazi, Joseph Machali na kumfukuza nyumbani kwake, akidai ni mlevi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alikiri mzee Machali kufungua jalada kumshitaki mwanawe.

Mtu aliyeshuhudia tukio hilo, alisema alimuona mzee huyo akiwa na fomu namba tatu ya polisi, huku akitembea kwa shida na mkono ukiwa umevimba kisha alipatiwa matibabu katika zahanati iliyoko jirani na wanakoishi.

Hata hivyo, akizungumza kwa simu kutoka Kasulu, mbunge huyo alikana kumpiga mzazi wake, na
kuongeza kuwa hizo ni propaganda za kisiasa zinazolenga kumchafua.

“Ni uzushi, kuna wana-CCM wanajaribu kunichafua kutokana na kuelemewa kisiasa. Mzee anaishi kwangu na hata leo yuko kwangu. Waeleze CCM watafute ajenda nyingine na si kufanya propaganda za mambo wasiyoyajua,”
 alisema.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya wana-CCM wamemshawishi baba yake akamshitaki kuwa amempiga na wamefanya hivyo kwa kutumia udhaifu wake wa ulevi naye alifanya hivyo.
“Yote yaliyofanywa hayakuwa ya kweli, alipogundua wanamtumia kisiasa amewakana na hakuna kesi yoyote polisi,” 
alisema.

Hata hivyo, alikiri kukerwa na tabia ya ulevi ya baba yake, ambaye amekuwa akimshauri kuacha kunywa pombe.

Mbunge huyo anadaiwa kumpiga baba yake Julai 15, mwaka huu, na kwamba mzee huyo alikwenda nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwilamvya, Dickson Joaqim, ambaye alimpeleka kituo cha polisi wilaya ya Kasulu kwa usalama zaidi.

Mzee huyo inaelezwa alichelewa kurudi nyumbani na alipomgongea mwanawe ndipo alipompiga kutokana na adha ya ulevi wake.

Imenukuliwa kutoka gazeti la Raia Tanzania.