Mhamiaji haramu akamatwa na mitambo ya kutengeneza fedha bandia

Raia wa Kongo, Ambanipo Siva (33) jana alikiri mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Frank Moshi mashitaka aliyosomewa na Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, Patrick Ngayomela kuwa anaishi nchini bila kuwa na kibali.

Hata hivyo Wakili Ngayomela alishindwa kumsomea maelezo ya awali, kwa kuwa alidai mshitakiwa huyo alipokamatwa, alikutwa akiwa na mitambo ya kutengenezea dola bandia za Marekani.

Wakili Ngayomela aliiomba Mahakama iruhusu mshitakiwa arudishwe Polisi ili ahojiwe waone kama watamuongezea mashitaka au la. Hakimu Moshi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12 mwaka huu, kesi itakapotajwa tena. 

Awali, Ngayomela alidai Julai 24 mwaka huu katika eneo la Mbezi Beach Wilaya ya Kinondoni, Siva alikutwa akiishi nchini bila kuwa na kibali. Alirudishwa rumande.

via HabariLeo