"Mimi ninaona ufanyike uchunguzi. Mwanafunzi aliyepata B, mwaka jana angepata C na nina shaka waliopata A” - Olouch

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Olouch akizungumza na gazei la Mwananchi Jumamosi ameshangazwa na ufaulu wa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu na kusema hakuna haja ya kufurahia matokeo haya bali kunahitajika uchunguzi.
“Tunahitaji kuchunguza zaidi kwa matokeo haya kwa nini ufaulu uongezeke hivi, hatuhitaji kuwa na majibu rahisi tu, kule kubadilika kwa mgawanyo wa alama kumechangia kwa kiasi kikubwa matokeo kuwa hivi.”: “Mfano mwanafunzi aliyepata alama B mwaka huu, kwa mfumo wa mwaka jana angepata alama C na nina shaka kwa waliopata A. Mimi ninaona ufanyike uchunguzi.”

Naye Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Loyola jijini Dar es Salaam, Porntian Kashangashi alisema ufaulu huo unaweza kuwa umetokana na mabadiliko ya upangaji wa madaraja:
“Unaweza kuwa labda mtihani ulitungwa kwa kupanua wigo kwa wengi wafanye vizuri au vibaya, lakini mimi ninavyojua unapotunga mtihani unaweka swali gumu moja na rahisi moja sasa kwa mtihani huo sijui ulikuwaje.”