Mpango wa hati punguzo wasitishwa sababu ya udanganyifu

Mpango wa hati punguzo ambao wajawazito na watoto wachanga, walikuwa wakigawiwa vyandarua bure, umesitishwa kutokana na kile kilichoelezwa ni udanganyifu, unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watumishi.

Mpango huo ulioanza mwaka 2004 , umesitishwa mwezi uliopita baada ya serikali kwa kushirikiana na wadau wake, ikiwemo shirika lililokuwa likiusimamia, kugundua kuwepo udanganyifu mkubwa.

Mpango huo ulianzishwa kuhakikisha wajawazito na watoto wachanga, wanaendelea kupata vyandarua vyenye viuatilifu kwa gharama nafuu, kuwakinga na maambukizi ya malaria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe waligundua udanganyifu mkubwa wa utekelezaji mpango hasa wa
kielektroniki, uliosababisha watu wasio walengwa kupata vyandarua na kuviuza.

Naibu Waziri alisema:
“Udanganyifu huo umefanywa na baadhi ya watumishi wa serikali na maduka binafsi wasio waaminifu kwa kutoa hati hewa kwenye mfumo wa kutoa chandarua kwa watu ambao siyo walengo wa mpango kisha kujipatia fedha isivyo halali,”
“Serikali ya Uingereza ambao ndio wafadhili wa mpango kwa sasa, wamesitisha ufadhili huo. Jambo hili ni la kusikitisha na halikubaliki,”
“Serikali inachukua hatua za dharura na madhubuti, kukabiliana nalo kwa kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kinidhamu kwa wale wote watakaothibitika kuhusika na wizi huu.”

Dk Kebwe alisema jambo hili ni la kusikitisha na halikubaliki, hivyo serikali inachukua hatua za dharura na madhubuti, kukabiliana nalo kwa kufanya uchunguzi wa kina kuchukua hatua za kinidhamu kwa wote watakaothibitika kuhusika na wizi huo.

Shirika la Mennonite Economic Development Associates (MEDA), ndilo lilikuwa likisimamia utekelezaji wa mpango huo.

Hata hivyo, Naibu Waziri alisema wanafanya majadiliano na Serikali ya Uingereza kupitia Idara yake ya Maendeleo (DFID), kuandaa utaratibu mpya vyandarua.

Alisema wameonesha nia ya kushirikiana na serikali katika utaratibu huo mpya, utakaotayarishwa, lengo likiwa ni kupambana na ugonjwa wa malaria. Aliomba umma uondoe wasiwasi, akisema vyandarua vitaendelea kutolewa kama ilivyopangwa.

Kulingana na maelezo ya Dk Kebwe, wamepanga Aprili mwakani mpango mpya utakapoanza, kuwe na utaratibu mpya wa ugawaji wa vyandarua hivyo vyenye viuatilifu vya muda mrefu usioruhusu mianya ya udanganyifu.
"Tumetayarisha rasimu kwa ajili ya utaratibu huo katika jamii kulingana na tafiti zilizopo, rasimu hiyo itaainisha na kuhakikisha mafanikio yanakuwa endelevu hususani kusambaza vyandarua kupitia kliniki ya mama na mtoto,"
alisema.

Rasimu hiyo ya utaratibu wa usambazaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu, itaainisha na kuhakikisha mafanikio yanakuwa endelevu hususani kusambaza vyandarua kupitia kliniki ya wajawazito na watoto, mifumo ya bima ya afya, kupitia wanafunzi shuleni na sekta binafsi.

Mpango huo ulikuwa ukichangia vyandarua milioni mbili kila mwaka kwa ajili ya wajawazito na watoto wachanga.

Serikali imesisitiza maandalizi ya mpango mpya kuziba pengo, litakalotokana na kusitishwa kwa huo uliokuwa ukifadhiliwa na Meda. Imesema katika mpango ujao, jamii yote itanufaika.

Mpango huo unaokuja, utaendelea kunufaisha wajawazito. Pia kutakuwa na ugawaji vyandarua kwa wanafunzi shuleni; mpango ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2013 kwa mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara.

Kupitia mpango huo uliositishwa, vyandarua milioni 13 vimesambazwa na kuchangia ongezeko la matumizi ya vyandarua kwa wajawazito kutoka asilimia 16 mwaka 2004 hadi asilimia 75 mwaka 2012 na kutoka asilimia 16 hadi 76 kwa upande wa watoto.

Mpango wa Hati Punguzo ulikuwa ukitekelezwa na Serikali ikishirikiana na sekta binafsi, hususani maduka ya reja reja na wazalishaji wa vyandarua na wadau mbalimbali.

Wajawazito walikuwa wakipata hati punguzo, wanapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza ya ujauzito husika. Watoto hupata hati wakati wanapohudhuria kliniki kwa ajili ya kupata chanjo.

Hati hiyo ilimwezesha mjamzito na mtoto wake, kupata chandarua kwenye duka teule kwa Sh 500. Aidha, serikali kwa kushirikiana na wadau wake ilikuwa ikilipia gharama kamili ya chandarua husika.

Hata za aina mbili zilikuwa zikitumika katika utekelezaji wa mpango huo; nazo ni hati ya karatasi iliyotumika tangu mwanzo wa mpango mwaka 2004 na hati ya kielektroniki iliyoanza mwaka 2011/12 hadi mwezi uliopita kabla ya mpango kusitishwa.