![]() |
Isaack Shayo, aliyefanya vizuri kitaifa katika masomo ya Sayansi |
Mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya Sayansi, Isaack Shayo ameweka wazi mbinu alizozitumia kufanikisha ufaulu wake.
Akizungumza na gazeti la HabariLeo na NIPASHE jana nyumbani kwao jijini Dar es Salaam, Isaack (20) ambaye alihitimu Shule ya Sekondari ya St Joseph’s Cathedral alisema, pamoja na mbinu nyingine, aliwasumbua walimu kutafuta maarifa na pia alihangaika kujitafutia vitabu.
Isaack yumo kwenye kundi la watahiniwa 10 bora kitaifa kwa masomo ya Sayansi na pia kwenye kundi la wavulana bora kitaifa katika masomo hayo.
Kijana huyo ambaye alikuwa akichukua masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabatu (PCM), alisema aliamini anaweza kufaulu lakini hakufahamu ni kwa alama zipi. Katika matokeo yaliyotangazwa jana, amepata alama 4. Fizikia amepata B+, Kemia A, Hisabati A pamoja na Sayansi ya Kompyuta (somo la ziada) amepata A.
Alisema chanzo cha yeye kupata ufaulu huo ni kujituma katika kusoma na pia kutafuta vitabu mbalimbali na pia kusumbua walimu alipoona amekwama.

"Nimefurahi sana lakini pia mbali na kufanya hayo yote pia kumwomba Mungu na kusali sana pia naamini kumenisaidia kuweza kupata matokeo haya mazuri,"
alisema Isaack.
Isaack alisema pia walimu waliomfundisha wamechangia kutokana na ufundishaji mzuri.
Alisema ndoto yake ni kuwa Mhandisi wa Ujenzi na anaamini atafanikiwa.
Akizungumzia changamoto alizokumbana nazo katika kusoma, alisema miongoni ni kutokuwepo vitabu vya Kidato cha Tano na Sita vya hapa nchini. Kwa mujibu wake, alilazimika kujisomea vitabu mbalimbali alivyoona vinahusu masomo anayochukua vikiwemo vya nje ya nchi
“Lakini nilijitahidi sana kusoma vitabu vingi ambavyo vipo pale kwenye maktaba ya shule kwa kuhakikisha nakuwa napata kile ninachokitaka,"
aliongeza Isaack.
Alisema hakuna jambo la ziada zaidi ya kusoma, kuwasumbua walimu na kusali yaliyomfanya afanye vizuri.
Kijana huyo anashauri wanafunzi wengine kuhakikisha wanafuata mambo hayo ambayo yanaweza kuwapa matokeo mazuri katika masomo yao.
Kwa upande wake, mama mzazi wa Isaack, Jane Mgaya alisema, mtoto huyo ni mtulivu na mwelewa.
Kwa mujibu wa mama huyo ambaye ni Katibu Muhtasi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hata wakati mtoto wake akiwa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Filbert Bayi, aliongoza kwa kuwa mwanafunzi bora.
“Hata alipokuwa Kidato cha Nne pia alifaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza. lakini jambo lingine alikuwa ni mtundu sana unaweza ukamnunulia mdoli wa ndege lakini ukakuta amefungua yote. Unagombana naye kwa kudhani ameharibu lakini baadaye anarudisha kama ilivyo,"
alisema Jane. (via HabariLeo)

Akizungumza na NIPASHE jana katika mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwao Mbezi Goig, Shayo alisema kuwa kusoma sana vitabu mbalimbali vya sayansi, ubora wa walimu shuleni kwao na kuhudhuria kwake masomo mengi ya ziada 'tuition' ni miongoni mwa sababu za kufanya vizuri.
“Kwakweli namshurku sana Mungu. Mtihani niliuona wa kwaida sana na hivyo kuamini kuwa ni lazima nitafaulu... lakini siyo kwa kiwango hiki. Nimefurahi sana kwa sababu najua kuwa sasa nina kazi ya kuongeza nguvu zaidi ili kutimiza ndoto yangu ya kuwa mhandisi wa majengo,"
alisema Shayo aliyezaliwa Dodoma mwaka 1994.
Akizungumzia maisha yake ya shule, alisema alianza darasa la kwanza katika Shule ya St. Mary mwaka 2001 na mwaka 2005 alihamia Shule ya St. Patrick darasa la sita na baadaye akamalizia darasa la saba shule ya Filbert Bay kabla kujiunga na sekondari ya Alpha.
Katika matokeo ya kidato cha nne, alisema alifaulu daraja la kwanza kwa kupata pointi 13."Nilipangiwa kidato cha tano katika Shule ya Vipaji Maalum ya Tabora Boys, lakini wazazi wangu wakanipeleka St.Joseph’s Cathedral," alisema.
Shayo alisema nje ya masomo yake anapendelea kusikiliza muziki, kuangalia filamu na pia anapenda soka, ingawa yeye siyo mchezaji na anaipenda timu ya Manchester United ya England na anampenda mchezaji Robin Van Persie 'RVP'. Anapenda pia muziki wa kizazi kipya na ni shabiki wa Joh Makini.
Chakula anachopenda ni wali samaki na kinywaji chake ni maji ya matunda.
Akizungumzia maisha yake ya shule, alisema alianza darasa la kwanza katika Shule ya St. Mary mwaka 2001 na mwaka 2005 alihamia Shule ya St. Patrick darasa la sita na baadaye akamalizia darasa la saba shule ya Filbert Bay kabla kujiunga na sekondari ya Alpha.
Katika matokeo ya kidato cha nne, alisema alifaulu daraja la kwanza kwa kupata pointi 13."Nilipangiwa kidato cha tano katika Shule ya Vipaji Maalum ya Tabora Boys, lakini wazazi wangu wakanipeleka St.Joseph’s Cathedral," alisema.
Shayo alisema nje ya masomo yake anapendelea kusikiliza muziki, kuangalia filamu na pia anapenda soka, ingawa yeye siyo mchezaji na anaipenda timu ya Manchester United ya England na anampenda mchezaji Robin Van Persie 'RVP'. Anapenda pia muziki wa kizazi kipya na ni shabiki wa Joh Makini.
Chakula anachopenda ni wali samaki na kinywaji chake ni maji ya matunda.
MZAZI AFICHUA SIRI YA BINTI ALIYEONGOZA
Mzazi wa msichana Doris Atieno Noah wa Shule ya Wasichana ya St. Marian Girls, ambaye amekuwa wa pili katika masomo ya Sayansi, amesema siri ya kufaulu kwa mwanawe ni juhudi, kuwa na malengo na pia kumtanguliza Mungu katika kila jambo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, baba wa Doris aitwaye Atieno Noah, amesema kuwa siku zote, binti yake amekuwa msikivu, mwenye kuzingatia maadili ya kanisa lao la Anglikana na pia amekuwa akijituma sana katika masomo kwa nia ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi wa umeme.
Na kwa sababu hiyo, Noah anasema Doris amekuwa akifanya vizuri kila anakopita na hivyo, hata matokeo yake ya sasa hayamshangazi sana.
"Labda kitu kipya kwake ni huku kuwa wa kwanza... lakini kwa ujumla familia yangu yote tumekuwa tukijua kuwa ana uwezo mkubwa sana darasani,"
anasema Noah, ambaye pia ana watoto wengine wanaosoma darasa la kwanza na la saba.
"Ninachoshukuru ni kwamba siku zote amekuwa mtoto mwema. Ni msikivu na daima amekuwa akipenda sana somo la mathematics (hisabati) kwa sababu anaamini kuwa ni kwa kufaulu vizuri somo hilo ndipo atakapoweza kutimiza ndoto yake ya kuwa injinia wa umeme,"
anasema Noah.
"Hata katika mitihani yake ya kidato cha nne alifanya vizuri sana na kuwamo katika orodha ya wasichana kumi bora kitaifa... alichaguliwa kwenda katika shule ya vipaji maalum ya Msalato (Dodoma). Hata hivyo, tukaamua kumpeleka St. Marian (Bagamoyo) kwa kuamini kuwa huko kutamsaidia kutimiza malengo yake.
Alipomaliza kidato cha nne na kufaulu kwa alama A katika masomo yote ya Sayansi, nilijaribu kumshauri achukue mchepuo wa PCB. Hata hivyo, alinikatalia kwa kusema kuwa angeweza kufanya hivyo, lakini asichotaka ni kusoma mchepuo usiokuwa na somo analolipenda sana la Mathematics.
Hivyo akabaki kusoma PCM (Fizikia, Kemia na Hisababati) na sisi tukaendelea kumuunga mkono ili aendeleze ndoto zake za kuona kuwa siku moja anakuwa injinia mzuri wa umeme,"
anasema Noah.
"Sasa tunashukuru kuona kuwa amefanya vizuri sana... shukrani kwa jitihada zake, shukrani kwa walimu wake na kubwa zaidi, shukrani kwa Mungu,"
anaongeza Noah, mfanyakazi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambaye pia hujishughulisha na kilimo cha alizeti. (via NIPASHE)