Mwanafunzi mbaroni kwa utapeli akijidai "Ofisa Mpelelezi"

POLISI mkoani Rukwa inamshikilia mwanafunzi wa udereva katika Chuo cha Furaha Center katika eneo la Kantalamba Manispaa ya Sumbawanga, Clever Simfukwe (19) kwa tuhuma za kujifanya Ofisa Mpelelezi wa Polisi katika mikoa ya Rukwa na Mbeya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Frednand Rwegasira alisema Simfukwe alikamatwa jana saa 3:00 asubuhi akiwa karibu na Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Sumbawanga akiwa amechanganya mavazi ya sare ya polisi na nguo za kiraia.

Akizungumzia undani wa kukamatwa kwake, Rwegasira alidai kuwa ni kutokana na kupata taarifa za
raia wema waliomtilia mashaka mtuhumiwa huyo kutokana na kukamata idadi kubwa ya wakazi wa mjini hapa ambao aliwalazimisha kumlipa fedha na kuwaachia huru kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kuwafikisha katika kituo cha polisi.
“Baada ya kukaguliwa nyumbani kwake alikokuwa anaishi na mpenzi wake katika kitongoji cha Chanji, Manispaa ya Sumbawanga alikutwa na sare za Jeshi la Polisi, kisu cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na Kujenga Taifa (JWTZ),"
alisema na kuongeza:
"Pia tulimkuta na mkanda wenye nembo ya bendera ya Jeshi la Polisi na pikipiki yenye nambari za usajili T 586 CNS aliyokuwa akiitumia kuwakamata madereva bodaboda na kuwalazimisha kumpatia fedha ili awaachie huru."

Rwegasira, ambaye hakuwa tayari kutaja jina la mpenzi wa mtuhumiwa huyo, alieleza kuwa alipohojiwa alikiri kuishi naye kinyumba ambapo alikuwa amemweleza kuwa yeye (mtuhumiwa) ni ofisa upelelezi wa Polisi.

Mwanamke huyo alidai kuwa mtuhumiwa alikuwa akimdanganya kuwa yupo likizo kumbe alikuwa akienda kukaa kwa baba yake mzazi ambaye ni Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Kasanga mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo.

Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lake utakapokamilika.

Katika tukio lingine, wakazi wawili wa jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na Polisi wakiwa katika harakati la kuuza gari linalosadikiwa kuwa ni la wizi.

Rwegasira alidai kuwa watu hao ambao hakuwa tayari kutaja majina yao kwa kuwa watavuruga ushahidi walikamatwa saa 7:00 mchana wakiwa katika harakati ya kuliuza gari hilo aina ya Toyota RAV4 yenye namba za usajili T 258 AYG katika eneo la Stendi Kuu mjini hapa.
“Sasa mteja aliwashtukia baada ya kuwatilia shaka na kubaini kuwa gari hilo halikuwa na vielelezo vyovyote vile wala jalada ndipo akatutaarifu na tukafanikiwa kuwatia mbaroni," 
alisema.

Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.