Polisi yawahoji Madaktari wa IMTU kuhusu mabaki ya miili ya watu


CP Suleiman Kova akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo wakati akitoa taarifa ya tukio la kukutwa kwa viungo vya binadamu liliyotokea jana jioni jijini humo.

Madaktari wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha kufunza Teknolojia ya Tiba na Utabibu (International Medical and Technological University  - IMTU) ni miongoni mwa watu wanaposhikiliwa na polisi kutokana na utupaji wa mabaki ya binadamu bila utaratibu.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema baada ya uchunguzi
iligundulika viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya chuo kikuu hicho ambacho pia hufanya mafunzo kwa vitendo.
“Baada ya kuwahoji walikubali kuhusika na utupaji wa viungo hivyo na kuwakamata kwa ajili ya uchunguzi zaidi kujua kwa nini walivitupa kwa wingi kiasi hicho kwa wakati mmoja na siyo kuvihifadhi au kuharibu ikiwa walivitumia kwa ajili ya mafunzo,”
alisema Kova.

Alisema katika eneo hilo, pia vilikutwa vifaa vinavyotumika hospitalini kama vile mipira ya kuvaa mikononi, mifuko miwili iliyotumika, nguo maalumu zipatazo 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.

Kamishna Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa viungo hivyo vilivyokamatwa vilikuwa ni vya maiti ambao hutumika na madaktari kwa elimu ya matibabu na utafiti. Polisi inaendelea kuwahoji na kufanya uchunguzi kuona kama wahusika wamefanya kosa linalohitaji kuchukuliwa hatua za kisheria au hawana kosa.

Ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeshafungua jalada la uchunguzi kubaini ikiwa wahusika wametenda kosa linalohitaji kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi. 

Amesema kuwa katika kutekeleza jambo hilo, tayari jopo la wataalamu 7 likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jaffar Mohamed linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha watu hao kutupa viungo hivyo katika eneo hilo na idadi ya watu kulingana na viungo vilivyotupwa.

Kova alisema siku hiyo ya tukio, wananchi wasiopungua 1,000 walifika katika eneo hilo na hakuna aliyefahamu vilikotoka ndipo walitoa taarifa polisi.

Kova alikanusha taarifa za kulihusisha gari jeupe aina ya pick-up lililokuwa limebeba mifuko ya plastiki na tukio hilo, badala yake, amesema gari hilo halihusiki. Amesema baada ya kuliona na kusikia harufu kali ikitoka humo, walioliona likielekea dampo wakadhani ni mojawapo ya magari yaliyobeba viungo hivyo.
"Wananchi wakalifukuza gari na walipomkamata dereva wakamlazimisha arudi dampo, akawa hana jinsi ila kwenda kituo cha polisi Bunju kujisalimisha...", "Zogo kubwa likafumuka kituoni hapo kiasi cha kuwalazimu polisi kutumia nguvu za wastani na kufanikiwa kuwatawanya wananchi hao..." "Huyu dereva alikuwa kabeba mabaki… ila siyo ya binadamu… Alikuwa kabeba mabaki ya kuku akitokea kiwanda cha kuku cha Interchick,"
alifafanua Afande Kova na kuzua kichezo cha mshangao kutoka kwa waandishi wa habari hao.


Aidha, amewasihi wananchi wasiwe na wasiwasi kwani viungo vilivyookotwa havina uhusiano na mauaji ya watu wengi na wala havihusiki na masuala ya ushirikina. Ameahidi kutoa taarifa kamili mara tu upepelezi utakapokamilika.

Jana jioni polisi ilitaarifiwa kuwapo kwa mifuko 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu katika maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji, eneo la Bunju, Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Mara baada ya kugunduliwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni walivichukua na kuvipeleka katika Hospitali ya Taifa kwa uchunguzi zaidi.