Raia Mwema: FBME inamilikiwa na kaka wawili wa familia moja kinyume cha taratibu za kibenki hapa nchini

BENKI ya FBME inamilikiwa na kaka wawili wa familia moja kinyume cha taratibu za kibenki hapa nchini, Raia Mwema limebaini.

Benki hiyo ambayo wiki hii imetawala katika vyombo vya habari baada ya kutuhumiwa na serikali ya Marekani kufadhili ugaidi, ndiyo benki inayotajwa kuwa na ukwasi mkubwa kuliko zote hapa nchini.

Ndugu wawili wanaomiliki benki hiyo ni Ayoub-Farid Michel Saab na Fadi Michel Saab, wanaomiliki asilimia 50 ya hisa kila mmoja katika benki hiyo ambayo mwaka jana ilikadiriwa kuwa na ukwasi unaofikia kiasi cha dola milioni 2.76 za Marekani (shilingi trilioni nne).

Kwa mujibu wa sheria za kibenki zinazotumika hapa nchini, benki hairuhusiwi kuwa na wamiliki wanaotoka katika familia moja kwa sababu ya kupunguza hatari ya familia kukubaliana kuanya tukio lenye hasara kwa sababu za kifamilia tu.

Gazeti hili limeelezwa na vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya BoT kwamba FBME haijakidhi
masharti ya umiliki wa benki hapa nchini yanayotaka taasisi hizi zimilikiwe na wana hisa mbalimbali na si watu wa familia moja.

“Hii benki inamilikiwa na watu wa familia moja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imelibaini hili na inalifanyia kazi. Tayari benki hii imetakiwa kuhamisha makao makuu yake kutoka Tanzania na kwenda kwenye nchi ambazo zinaruhusu kitu hicho.

“Inachoweza kufanya benki hii kwa sasa ni kuhamisha ofisi zake za makao makuu kutoka Tanzania na kwenda katika nchi nyingine. Nasikia wana mpango wa kuhamia Mauritius.

“Kama makao makuu yake ni sehemu nyingine, benki inaruhusiwa kufanya kazi hapa nchini hata kama wamiliki wake ni watu wasio wa familia moja. Lakini haiwezi kufanya hivyo ikiwa makao yake makuu ni Tanzania,” kilisema chanzo kimoja cha kuaminika cha gazeti hili.

Benki ya FBME ina matawi manne tu nchini Tanzania ambayo yako katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar.

FBME ilianzishwa mwaka 1953 nchini Lebanon, Mashariki ya Kati, ikitumia jina la Federal Bank of Lebanon (SAL) na ilihamishia makao yake makuu nchini Tanzania mwaka 2003 ikitokea katika visiwa vya Cayman.

Visiwa vya Cayman pamoja na Cyprus vimetajwa mara nyingi kama mojawapo ya maeneo yanayofahamika zaidi kwa jina la Pepo za Wakwepa Kodi (Tax Havens) kutokana na kutoza kodi kidogo au kutotoza kabisa kwa wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa.

BoT imekuwa wakali katika uangalizi wa mabenki hapa nchini na ndiyo maana tangu kufilisika kwa benki ya Greenland hapa nchini, tukio kama hilo halijawahi kutokea tena; ingawa kwa Afrika, wastani ni kuanguka kwa benki moja walau kila mwaka.

Wakati huohuo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, amesema Watanzania wote wenye akiba katika benki ya FBME hawatapoteza fedha zao kwa sababu tatizo la benki hiyo si la kifedha.

Akizungumza na Raia Mwema jijini Dar es Salaam wiki hii, Ndullu alisema matatizo ya benki hiyo kuhusishwa na ugaidi hayana uhusiano na ukosefu wa fedha.

“Mimi ningewaambia Watanzania kwamba hawana sababu ya kuhofu kwamba wataweza kupoteza fedha zao endapo tatizo lolote litaikuta hii benki. Kinachotokea ni suala la kawaida.

“Huu uangalizi ambao tunaufanya sasa ni jambo la kawaida kwa benki zote. Kimsingi, kila siku tunazikagua benki kutokana na taarifa mbalimbali ambazo tunazo.

“Kama tatizo la FBME lingekuwa ni la kifedha, hapo kungekuwa na sababu ya watu kuwa na hofu. Lakini hali ya kifedha ya FBME ni nzuri na hakuna sababu ya watu kuwa na hofu,” alisema Ndullu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, serikali ya Marekani iliituhumu FBME kwa kuhusika na utoroshaji wa fedha, ufadhili wa ugaidi na kujihusisha katika vitendo viovu.

Hali hiyo ilizusha taarifa kuwa benki hiyo itafungwa na wateja wake kupoteza amana walizoziweka katika benki hiyo.

Marekani inadai kwamba kiasi cha dola milioni 875 (Shilingi bilioni 147) zimepitishwa katika benki hiyo yenye makao yake makuu nchini Tanzania katika namna yenye kutia shaka.

FBME ina mali nyingi zaidi nchini Cyprus na kwa mujibu wa taarifa ya Marekani, zaidi ya asilimia 90 ya malipo mbalimbali yanayofanyika katika benki hiyo, hutokea katika taifa hilo.

- See more at: Raia Mwema