Raia Mwema lazungumza na Balozi wa Norway kuhusu gesi ya Tanzania

SERIKALI ya Norway imevunja ukimya wake kuhusu suala la kampuni yake ya StatOil kuingia mkataba wa gesi na mafuta na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ambao ni kinyume cha mkataba wa mfano (Model PSA).

Balozi wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik, aliliambia Raia Mwema jijini Dar es Salaam wiki hii kwamba serikali yake imesikia kuhusu malalamiko ya mkataba huo lakini akasema “suala hilo ni la kibiashara na litamalizwa kibiashara.”
“Tumesikia kuhusu hayo malalamiko lakini StatOil, japo inamilikiwa na serikali kwa kiwango kikubwa, inajiendesha kibiashara na ndiyo sababu ya kuwa miongoni mwa kampuni zenye faida zaidi ulimwenguni katika sekta hiyo.
“Makubaliano yoyote ambayo yamefanyika baina yaTPDC na StatOil yalikuwa ni ya kibiashara na serikali ya Norway haikuhusika kwa lolote. Kama upande wa Tanzania unaona kuna mapungufu, basi iwasiliane na mwenzake ili hatimaye mwafaka ufikiwe.” 
Kauli ya Balozi huyo ni ya kwanza kutolewa na serikali ya Norway au StatOil wenyewe tangu
kuvuja kwa mkataba huo kwenye mitandao ya kijamii mapema mwezi huu.

Norway ni miongoni mwa nchi zinazochangia sana katika mafunzo ya kusaidia Watanzania kufaidika na utajiri ilionao kwenye eneo la mafuta; na uingiwaji wa mkataba huu unaleta utata katika dhamira haswa ya taifa hilo kwenye sekta changa ya nishati hapa nchini.

Tanzania inatarajiwa kupoteza mabilioni ya shilingi kutokana na kusaini, kupitia TPDC, Mkataba wa Kutafuta na Kuzalisha Gesi Asilia (PSA) ambao unaipa kampuni hiyo ya kigeni mapato makubwa kinyume cha namna mikataba hiyo inavyotakiwa kuwa kwa mujibu wa serikali yenyewe.

Kwa mujibu wa mkataba wa mfano, ambao umewekwa hata kwenye tovuti ya TPDC, mikataba hiyo imegawanyika katika sehemu mbili; Mosi wakati uzalishaji unapokuwa wa chini na pili wakati uzalishaji unapokuwa wa juu.

Mkataba wa mfano unaeleza kwamba wakati uzalishaji ni mdogo, mwekezaji atakata gharama zake zote za uzalishaji na kilichobaki kitagawiwa sawa baina yake na TPDC.

Mkataba huo unaeleza pia kwamba wakati uzalishaji unapokuwa mkubwa, mwekezaji atakata gharama zake na kilichobaki kitagawanywa kwa serikali kupata asilimia 80 ya mgawo huku mwekezaji akipata asilimia 20.

Mkataba huo wa mfano umeweka wazi kwamba mwekezaji anaweza kujilipa hadi asilimia 70 ya gesi yote inayozalishwa kama gharama zake za uzalishaji na hivyo kimsingi kinachogawiwa baina ya serikali na mwekezaji ni asilimia 30 tu.

Hata hivyo, mkataba uliovujishwa unaonyesha kwamba wakati uzalishaji ukiwa chini, StatOil itapata asilimia 70 huku TPDC ikipata asilimia 30 na wakati uzalishaji ukiwa juu, wabia wanapata kiasi sawa.

Hii maana yake ni kwamba katika kila uniti 100 ya gesi itakayozalishwa, StatOil kwanza atapata uniti 70 za kufidia gharama na uniti 15 nyingine (sawa na uniti 85) huku TPDC (Tanzania ikiambulia uniti 15 tu; huku yenyewe pia ikitakiwa kulipia mrabaha kwa vile ndiyo yenye leseni ya kumiliki eneo.

Serikali, kupitia TPDC, haijaukanusha mkataba huo, isipokuwa imewapinga wakosoaji wake kwa madai kuwa wanapotosha suala hili.

Kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Yona Killaghane, TPDC ilisema kwamba kwenye suala hilo, Tanzania itafaidika katika mkataba huo kutokana na makusanyo ya kodi mbalimbali.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisema Serikali imefanya makosa kuingia katika mkataba huo kwani kama ingefuata mkataba wa mfano, TPDC ingepata uniti 24 katika kila 100 zinazouzwa badala ya uniti 15 itakazoambulia katika mkataba huu uliovuja.
----
Makala hii imenukuliwa kutoka katika gazeti la Raia Mwema