Raia Mwema: Vigogo wa Upinzani mbioni kutimkia...

KATIKA hatua itakayowatikisa vigogo wa Upinzani, wabunge kadhaa wa kambi hiyo wamo mbioni kuikimbia, Raia Mwema limeambiwa.

Wabunge hao wanatarajiwa kuhama vyama vyao vya sasa na kujiunga na chama kipya cha upinzani wakati wowote kuanzia kumalizika kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), taarifa zinasema.

Wengi wa wabunge hao wanatoka katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Mashariki na Ziwa Magharibi na gazeti hili limeambiwa kwamba maamuzi tayari yamekwishakufanyika, kinachobaki sasa ni tukio lenyewe.

Chama wanachotajwa kuhamia wabunge hao ni kile cha Alliance for Change and Transparency (ACT) kinachohusishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe.

Zitto mwenyewe hajahamia katika chama hicho lakini mmoja wa maswahiba wake kisiasa, Samson
Mwigamba, tayari amejiunga na ACT na tayari ameanza kufanya ziara za kisiasa katika baadhi ya mikoa.

Gazeti hili limepewa majina tayari ya baadhi ya wabunge ambao watahama kutoka katika vyama vyao vya sasa lakini kwa sababu maalumu, majina haya hayatatajwa kwa sasa.

Mmoja wa wabunge ambao wanatarajiwa kuhamia ACT amezungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita na amethibitisha kwamba atahama baada ya kumalizika kwa muda wake wa ubunge; yaani baada ya kuvunjwa rasmi kwa Bunge hili mwakani.

“Mimi naondoka. Kama nchi yetu ingekuwa inaruhusiwa mwanasiasa ku-cross (kuhamia chama kingine) bila ya kupoteza ubunge wake, ningekuwa tayari nimehama. Lakini siwezi kuhama kwa sasa.

“Nikihama, kwanza nitakosa fursa ya kushiriki katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ya Tanzania na pia kuchangia katika masuala ya kitaifa kupitia mijadala ya kibunge.

“Halafu kuna suala la kipato pia. ACT ni chama kipya na hakina chanzo chochote cha mapato. Kama Mbunge nitaendelea kupata mshahara wangu na pia kuchangia chama changu. Ni busara kubaki na ubunge kwanza,” alisema mbunge huyo.

Vyama ambavyo vinataraji kupoteza wabunge wake ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na NCCR-Mageuzi, huku ikidaiwa kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kinaweza tu kupoteza baadhi ya wanachama wake wa Tanzania Bara wenye nguvu ya ushawishi mikoani.

Raia Mwema limeambiwa kwamba hatua ya baadhi ya viongozi wa CHADEMA katika baadhi ya mikoa kutangaza kujitoa kwenye chama hicho kwa sasa, ni sehemu ya mpango uliopangwa vizuri wa watu kuondoka hatua kwa hatua.

Mmoja wa viongozi walioachia ngazi ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma, Jaffar Kasisiko, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Magharibi, Shaabani Mambo na Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma, Msafiri Wamalwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kwamba wana fununu kwamba wapo viongozi wengine wa chama hicho ambao wanajiandaa kuondoka.

Hata hivyo, gazeti hili linafahamu kwamba picha ya wabunge gani wataondoka katika vyama vya upinzani itajulikana zaidi baada ya Bunge Maalumu la Katiba ambapo wapo ambao wataanza kuonyesha dhahiri nia yao hiyo.

“ACT wana siri kubwa na itaanza kuwekwa wazi kuanzia baada ya BMK. Baada ya hapo kutakuwa na mikutano isiyozidi minne kabla ya Bunge kuvunjwa. Subiri kwanza BMK liishe,” alisema mbunge mwingine anayetajwa kupanga kuhama lakini asiyetaka kuhusishwa kabisa na ACT katika hatua ya sasa.

“Kaka, nakuomba sana usitaje jina langu wala kutumia picha yangu kwenye gazeti lako. Ukifanya hivyo utakuwa umenimaliza kabisa. Kwanza nashangaa mambo haya yamevujaje. Najua tu ni ….. (jina linahifadhiwa) ndiye amekuambia,” alisema Mbunge huyo wa sasa.

Lakini wengi wa wabunge na wanasiasa wanaotarajiwa kuhamia ACT wametajwa kuwa vijana wanaoona kwamba maisha yao kisiasa ndani ya chama hicho yatakuwa rahisi kuliko katika vyama ambavyo vimejijenga tayari.

Wakati mbunge huyo akizungumza na Raia Mwema, alikuwa na kijana mmoja anayejihusisha sana na siasa katika vyuo vikuu ambaye alimwambia mwandishi wa gazeti hili kwamba atakwenda ACT kwa vile tu “ hawezi kudandia katika basi lililojaa” –akimaanisha vyama vingine vikuu vya siasa hapa nchini.

Juhudi za gazeti hili kutaka kuzungumza na Mwigamba ili kupata uhakika kama kweli wanataraji kupata wabunge zilikwama baada ya mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa CHADEMA kusema hafahamu lolote.

“Mimi kwa kweli nasikia tu habari hizo kama wewe lakini sifahamu chochote. Sisi tunajenga chama na kama kuna watu ambao wanaamini katika tunachotaka kufanya, tutawakaribisha tu. Lakini hakuna kitu mpaka sasa,” alisema mwanasiasa huyo.

Zitto hakuweza kupatikana kutoa maoni yake kwa vile yuko safarini nje ya nchi kwa shughuli zake za kibunge.

- Raia Mwema