Serikali yaifunga Hospitali ya IMTU kwa muda usiojulikana


Taarifa ya TBC1 inapasha kuwa Serikali imeifungia kutoa huduma ya matibabu hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Utabibu na Teknolojia ya Tiba (IMTU) ya jiijni Dar es Salaam kwa muda usiojulikana.

Hatua hiyo inafuatia ripoti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza katika hospitali hiyo, na kubaini kuwa huduma zinazotolewa na hospitali hiyo zipo chini ya viwango na maadili ya utoaji matibabu hapa nchini.

Akitoa ripoti ya ukaguzi kwa uongozi wa hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni
Dk Gunini Kamba, amesema ukaguzi wao umebaini hospitali ya IMTU ina upungufu wa vitendea kazi ikiwemo kifaa cha kuchoma taka ngumu.

Mapungufu mengine ni pamoja na kutokuwa na wauguzi wa kutosha, kuchanganya dawa (zilizokwisha na zisizoisha muda wa matumizi) na wauguzi kufanya kazi zisizowapasa.

"Baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza tumebaini kuwepo kwa mapungufu haya, kwa hiyo tunaifungia hospitali hii mpaka pale watakaporekebisha," alisema Dk Kamba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya IMTU, Prof. Yasini Mgonda, amekiri kuwepo mapungufu katika Hospitali hiyo na kuahidi kufanyia kazi na kuiomba Manispaa na Wizara ya Afya kurejea adhabu hiyo.

IMTU inhusishwa na tukio la utupaji wa viungo vya binadamu vilivyotumika kwa mafunzo (cadaver) mithili ya takataka.