Serikali yazungumzia madai ya THTU na CWT kuhusu nia ya kupunguza mafao ya pensheni kwa Wanachama wa LAPF na PSPF

Mkurugenzi wa Sheria wa SSRA, Ngabo Ibrahim (katikati), akiandika taarifa hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka na Meneja Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Sarah Kibonde.

Na Dotto Mwaibale - SERIKALI imekanusha tamko liliotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisiza Elimu (THTU) na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) la kudai kwamba kuna mpango wa kupunguza Mafao ya Pensheni ya wanachama mifuko ya LAPF na PSPF.

Akizungumza Dar es Salaam leo Kamishna wa Kazi wa Wizara ya Kazi na Ajira, Saul Kinemela alisema taarifa hizo sio za kweli ambazo kwa namna nyingine zinalenga kupotosha umma.
"Tunaomba wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na umma kwa ujumla kuwa kinachoendelea ni majadiliano na wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii yenye lengo la kuboresha mafao ya wastaafu"
Alisema kuwa Chama cha Walimu Tanzania ( CWT) na THTU wakiwa ni wadau sekta ya hifadhi ya jamii wanayo haki ya kikatiba ya kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali yakiwamo ya sekta ya hifadhi ya jamii.

Alisema Serikali inachukua fursa hiyo kuwatoa hofu wastaafu na wanachama wote wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
"Tunaomba wadau wote wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa watulivu na kujiepusha na maneno yoyote ya upotoshwaji na mwisho kuwachanganya wanachama na hivyo kupunguza ufanisi wa kazi na utendaji"
Kamishna wa Kazi wa Wizara ya Kazi na Ajira, Saul Kinemela (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana , wakati akikanusha taarifa zilizotolewa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), zilizodai Serikali inampango wa kupunguza mafao ya Pensheni ya Wanachama wa Mifuko ya LAPF na PSPF. Kulia ni Kamishna wa Kazi Msaidizi, David Kanali na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Juma Muhimbi.