Taarifa ya kufukuzwa kwa Watumishi 9 na karipio kali - Manispaa Kinondoni


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Baraza la Madiwani la Manispaa yaa Kinondoni katika Kikao chake cha tarehe 22/07/2014 siku ya Jumanne, chini ya Mstahiki Meya Mh. Yusuph Mwenda pamoja na mambo mengine lilijadili na kutolea maamuzi ya mashauri ya mashtaka ya nidhamu yaliyofunguliwa kwa Watumishi 11 wa Idara mbalimbali za Manispaa waliofanya makosa mbalimbali kama Utoro kazini, Matumizi mabaya ya madaraka na ofisi.

Kati ya Watumishi 11 waliofunguliwa Mashtaka, watumishi 6 ni wa Idara ya Afya, 2 ni wa Idara ya
Elimu ya Sekondari (Walimu wa Leseni) na 3 ni wa Idara ya Utawala na Utumishi kada ya Maafisa  watendaji wa Mitaa ambao ni 2 na polisi msaidizi 1.

Aidha Baraza limefikia uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi 9 na kuwapa karipio watumishi 2. Kati ya watumishi 9 waliofukuzwa kazi, watumishi 4 ni wa Idara ya Afya, 3 Idara ya Utawala na Utumishi ambao ni Maafisa watendaji wa Mitaa 2 na Polisi Msaidizi 1, na 2 kutoka idara ya Elimu ya Sekondari ambao ni walimu wa Lesseni.

Watumishi 2 waliopewa karipio kutoka Idara ya Afya wametakiwa kujirekebisha, ambapo watakuwa katika uangalizi kwa muda kuona kama wamejirekebisha mienendo yao.

Baraza la Madiwani limewataka watumishi wote, kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali ya Serikali katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma kwa Umma sambamba na kuheshimu maadili ya kazi zao kwa hekima na busara, ili kuweza kutoa huduma bora kwa wakazi wa Kinondoni.

Aidha, Baraza limesisitiza kuwa halitasita na litaendelea kuchukua hatua za kinidhamu  kwa watumishi wanao fanya makosa mbalimbali.

IMETOLEWA NA:
SEBASTIAN MHOWERA
AFISA UHUSIANO
HALMASHAURI YA MANISPAA YA KINONDONI.