![]() |
Kaimu Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. James Andilile (kushoto) akijibu maswali toka kwa waandishi wa habari waliohudhuria Mkutano uliohusu Kampuni ya Statoil yenye mkataba wa kuchimba mafuta nchini Tanzania baada ya kutokea kwa mkanganyiko kwa baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari zilizokinzana kuhusu Kampuni hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. Yona Killagane. (picha: Benedict Liwenga/Maelezo) |
Na Winner Abraham -- SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa ufafanuzi kuhusiana na Kampuni ya Statoil, yenye mkataba wa kuchimba mafuta nchini Tanzania baada ya kutokea kwa mkanganyiko kwa baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari zilizokinzana kuhusu kampuni hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzani (TPDC) Bw. Yona Killagane ameeleza taarifa zilizo sahihi kuhusu kampuni ya Statoil na mikataba yake mbalimbali na Serikali katika upataji wa faida kutokana na utafutaji wa mafuta na gesi.
Killagane ameeleza kuwa utaratibu unaotumika katika kutafuta mafuta ni aghali na ni hatari kwa
maisha, hivyo Serikali haiwezi yenyewe kuingia gharama hizo za utafutaji na badala yake inatumia mifumo mbalimbali kama vile Concession agreement, Service agreement pamoja na Mkataba wa kugawana mapato ambapo kati ya mikataba hiyo mitatu Serikali inatumia mkataba wa kugawana mapato ambapo humpa mwekezaji kazi kisha rasilimali zikigunduliwa hugawana na kampuni hiyo au mwekezaji aliyegundua. Hivyo Serikali inategemea kupata mrahaba na kodi toka kwa makampuni inayoingianayo mikataba.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi huyo, amevieleza vyombo vya habari kuwa ugunduzi wa gesi unategemea miundombinu mingi na inategemea uwingi wa gesi hiyo ndiyo maana Serikali inaingia mikataba na makampuni makubwa yenye uwezo mkubwa wa kifedha ili kuweza kufanya utafiti na kuchimba mafuta na gesi.
Aidha, Bw. Killigane amefafanua kuwa mkataba walioingia kati ya Serikali na kampuni ya Statoil mwaka 2007, ulikuwa ni wa kutafuta mafuta na sio gesi lakini hapo mwaka 2012 mkataba mwingine wa kutafuta gesi ulifanyika kati ya kampuni hiyo na Serikali.
“Statoil ilipendekeza kuwa kwenye mgao wa mkataba wa mwanzo Serikali ipate asilimia 5% na Statoil asilimia 95% kama zabuni iliyokuwa imeletwa, lakini baadaye kamati ikakaa na kuzungumza na mwekezaji ambapo mwekezaji aliweza kusukumwa kutoka asilimia 5% hadi asilimia 30% na hivyo hii ilijumuisha TPDC kuweza kujiunga kwa asilimia 10%, kwa sasa katika mkataba wa mafuta serikali inapata asilimia 56% na Statoil asilimia 44%, katika mkataba wa wa gesi Serikali inapata asilimia 61% na mwekezaji asilimia 39% katika kipindi cha mkataba.”
Alisema Killigane.
Naye Kaimu TPDC Bw. James Andilile aliwahakikisha waandishi wa habari, kuwa Serikali iko tayari kusaidiana na waandishi wa habari katika kutoa taarifa sahihi ili kuweza kuwaeleza Watanzania kuhusiana na sekta ya mafuta na gesi na nini kinaendelea.
Naye Kaimu TPDC Bw. James Andilile aliwahakikisha waandishi wa habari, kuwa Serikali iko tayari kusaidiana na waandishi wa habari katika kutoa taarifa sahihi ili kuweza kuwaeleza Watanzania kuhusiana na sekta ya mafuta na gesi na nini kinaendelea.
“Hii nchi ni yetu na kazi zote tunazozifanya ni kwa ajili ya Watanzania, jinsi waandishi wa habari wanavyotoa taarifa zisizo sahihi wanaharibu sura ya nchi yetu na kuwapa hofu wawekezaji na hivyo kuleta hasara badala ya faida, kama kuna jambo lisiloeleweka tunawaomba kwa wakati wowote mkituita tutakuwa tayari kuwapa taarifa ili wote kuwa katika ufahamu mmoja”.
Alisema Andilile.
![]() |
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. Yona Killagane akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na Kampuni ya Statoil yenye mkataba wa kuchimba mafuta nchini Tanzania. |