Ufafanuzi wa TFDA kuhusu taarifa za uwepo sokoni wa dawa zilizoisha muda wa matumizi

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA

tfda tanzania logo


Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa zilizoripotiwa na gazeti la Tanzania Daima la kila siku kuhusu uwepo wa dawa zilizoisha muda wa matumizi kwenye duka la dawa la Core Pharmacy jijini Dar es Salaam. Taarifa hizi zimekuwa zikitolewa na mmiliki wa duka la dawa la Shine Care Pharmacy kwenye gazeti hilo. Baadhi ya dawa zilizotajwa ni Listerine antiseptic mouthwash, Pimple Gel, Misoprostol tablets 200mcg, Rabeloc IV 20mg, Mefenamic acidic tablets, Herpex – 800 DT, Inhaler 100 pg dose, Metformin Denk 850, Comprimes de carvediola 12.5mg na Cloderm cream.

Aidha, taarifa zimedai pia kuwa TFDA pamoja na kufahamishwa suala hili haikuweza kuchukua hatua zozote kwa mlalamikiwa.

TFDA inapenda kukanusha upotoshaji huo unaofanywa na chombo hicho cha habari kutokana na
ukweli uliopo. TFDA ilifuatilia suala hilo na kubaini uuzwaji wa dawa moja tu ya Listerine antiseptic mouthwash (chupa 2) ambayo iliuzwa katika kipindi ambacho muda wake wa matumizi ulikuwa umebaki mwezi mmoja. Taarifa zinazoendelea kutolewa na gazeti la Tanzania Daima zinatokana na mgogoro uliopo baina ya makampuni mawili ya kuuza dawa ya Core Pharmacy na Shine Care Pharmacy.

TFDA inauhakikishia umma kwamba iko makini na ina mifumo madhubuti ya kufuatilia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, chakula, vipodozi na vifaa tiba kwenye soko. TFDA inaviasa vyombo vya habari pia kufanya uchunguzi wa kina na kufika ofisini kwake ili kupata taarifa sahihi badala ya kutoa taarifa inazozipokea kutoka kwa wafanyabiashara.

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
S.L.P 77150, DAR ES SALAAM
Simu: + 255 222 450512/450751/452108
Nukushi: + 255 222 450793