Wachina waondoka na dhahabu wananchi wabaki na uharibifu

WACHINA walifika katika Kijiji cha Lupa Market wilayani Chunya, wakajizolea dhahabu, wakaondolewa, manufaa pekee kwa kijiji ilikuwa uharibifu mkubwa wa mazingira ya Mto Lupa na Zira huku wananchi wake wakiendelea kujichimbia kwenye umasikini.

Zaidi ya Wachina 13 walivamia Mto Lupa na Zira katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya. Wakiwa na mitambo ya kisasa, wakajichimbia dhahabu kwa gharama ya maisha ya Watanzania masikini waishio kwenye vijiji vilivyomo kwenye mabonde ya mito hiyo.

Wachina hao kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya Epoch Mining Tanzania Ltd waliweka mitambo minne; miwili katika kila mto. Mitambo hiyo ilikuwa ikielea majini mithili ya pantoni ambapo wenyeji waliita meli.

Hadi wanaondolewa, si serikali ya kijiji, wilaya wala mkoa waliokuwa na taarifa ya kiwango cha
dhahabu iliyozalishwa na Wachina wale, au kuambulia malipo yoyote kutokana na uzalishaji huo.

Si kudanganyia kwa kutoa msaada wa japo dawati moja wala kujenga japo chumba kimoja cha darasa, waliondoka na asilimia 100 ya walichokivuna.

Afisa Madini Mkazi Wilaya ya Chunya, Donald Mremi anakiri serikali kutopokea chochote kutoka kwa Wachina wale, iwe kodi ya huduma (service levy), mrabaha au kutoa huduma za kijamii kwa vijiji walikokua wakiendesha shughuli zao za uchimbaji dhahabu.

Katika mahojiano yake na Raia Mwema ofisini kwake, Mremi alithibitisha pia kuhusu uharibifu wa mazingira walioufanya.

“Walifanya uchafuzi mkubwa wa mazingira, hadi wanaondolewa walikuwa hawajalipa chochote,” anasema Afisa Madini huyo.

Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbulu anathibitisha halmashauri hiyo kutopokea malipo yoyote kutoka Kampuni ile ya Wachina iliyokuwa ikichimba dhahabu ndani ya mito Lupa na Zira.

Anabainisha kuwa utaratibu uliotumika miaka ya nyuma ulichangia mamlaka zilizopo maeneo zinakoendeshwa shughuli za uchimbaji madini kutofahamu chochote kuhusu uhalali wa makampuni hayo ya uchimbaji madini.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawilo anakiri pia kampuni hiyo ya Wachina kutofuata sheria na taratibu zilizopo zenye kutawala sekta ya madini, na kubainisha kuwa serikali wilayani humo itasimamia sheria, na yeyote atayekiuka, awe mwekezji toka nje au mwananchi wa kawaida ataondolewa.

“Wale tuliwatoa kwa sababu hawakufuata sheria na taratibu, sheria inasema mita 60 kutoka chanzo cha maji, lazima watu watii,” anasema Mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza, “ hata baada ya kuwaondoa Wachina, waliingia wananchi kuchimba, nilienda nikawaondoa.”

Walichoambulia wananchi wa Kijiji cha Lupa Market pamoja na Ifumbo, ni Mto Lupa na Zira kupungukiwa maji zaidi kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa na Wachina wale, na watoto wao kuendelea kusoma katika mazingira duni huku utajiri wao ukipelekwa kuendeleza watoto wa mataifa yao, tena yenye uchumi mkubwa duniani.

“Shule haikuwahi kunufaika chochote na dhahabu iliyochimbwa, japo walikubaliana na Halmashauri ya Kijiji wajenge madarasa, lakini hawakuwahi kutekeleza,” anasema Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Lupa Market.

Manufaa pekee yanayoelezwa kupatikana shuleni hapo kutokana na sakata la kampuni hiyo ya Kichina, ni kukamilishwa kwa vyumba viwili vya madarasa na kuifanya shule hiyo yenye darasa la kwanza hadi la saba kuwa na vyumba vine sasa.

Hatua ya kukamilishwa kwa vyumba hivyo vya madarasa ilitokana na picha iliyochapishwa kwenye Raia Mwema katika moja ya makala kuhusu Wachina hao kujizolea dhahabu kwenye Mto Lupa na Zila, ikionyesha watoto wakisomea chini ya mti huku wageni wakiondoka na mali kilometa nane tu kutoka kijijini hapo.

“Picha ile ilisaidia sana kusukuma kukamilishwa kwa vyumba viwili, tulishangaa kuona uongozi wa wilaya chini ya DC umefika shuleni, wakatoa shilingi 500,000 kukamilisha vyumba viwili,” anasema kiongozi mmoja kijijini hapo.

Mkuu wa Wilaya Kinawilo alipotakiwa kuzungumzia suala la shule alikiri kuikuta katika hali mbaya, hivyo kulazimika kutoa shilingi laki tano kumalizia vyumba viwili pamoja na kuzuia utaratibu wa wanafunzi kusomea chini ya mti.

“Nilikuta watoto wako chini ya mti nikasema watoke, pale ni hatari anaweza dondoka mjusi tu ikawa balaa, nashukuru umendelea kufuatilia suala la hiyo shule, umenikumbusha na mimi, ngoja niwasiliane na Mkurugenzi,” alisema Kinawilo.

Tukio la kampuni hiyo ya Kichina ni sehemu tu ya mwendelezo wa wageni, ikianzia enzi za kabla ya uhuru, kuingia katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, wakajizolea dhahabu na kuondoka, wilaya yenyewe ikiachiwa uharibifu mkubwa wa mazingira yake yakiwamo mashimo yaliyosambaa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Wakati Wachina wale wa mwaka 2010 wakiondoka na dhahabu kwenda kujenga kwao, Wilaya ya Chunya na wananchi wake wamendelea kuongelea kwenye dimbwi la umasikini, na watoto wao wakiendelea kusomea katika mazingira duni.

Miongoni mwa madhara yaliyowakabili wananchi wakati Wachina wale wakichimba dhahabu kwenye mito hiyo miwili ni pamoja na magonjwa yakiwemo ya kuharisha na ya ngozi, magonjwa yaliyoelezwa kusababishwa na shughuli hizo za uchimbaji ambapo mitambo yao iliyowekwa ndani ya mito, ilitumia mafuta na madawa, hivyo kuchafua maji.

Leo hii hali ni shwari, hakuna tena hayo magonjwa kama anavyothibitisha mwanakijiji wa Lupa Market, Alexander George akisema: “ Hakuna tena magonjwa yale ya kuhara, maji hivi sasa ni safi, wale Wachina walichafua sana maji, kulikuwa na mafuta, madawa na vinyesi.”

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa mazingira wilayani Chunya wanalitupia lawama Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wakisema mara baada ya kupitisha andiko la tathmini ya mazingira (EIA), huwa hawafanyi tena ufuatiliaji kuona kama mwekezaji anafuata yaliyomo kwenye EIA yao.

“NEMC wanapaswa kubeba lawama ya uharibifu wa mazingira wilayani Chunya, wao ndio wanafanya EIA, tatizo wanaweka taratibu vizuri, wanahakikisha kila kitu kipo sawa, lakini wakishapitisha na kulipwa hawafanyi tena ufuatiliaji, kwa hiyo wenye makampuni kuwa huru, wakifanya watakavyo,” anasema Lucas Malangalila ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali yenye kujihusisha na masuala ya mazingira wilayani Chunya ya Kalangali.

Kupitia Kampuni ya EPOCH Mining (T) Ltd Wachina hao waliendesha shughuli zao za uchimbaji dhahabu ndani ya mito hiyo kwa kutumia leseni Na. ML 207/2005 iliyotolewa Machi 10, 2005 kwa Kampuni ya KAMAKA CO. LIMITED ya jijini Dar es Salaam na waziri wa wakati huo wa Wizara ya Madini na Nishati, Daniel Yona.

Leseni hiyo ilihamishiwa kwa Kampuni ya EPOCH Mining (T) Ltd Desemba 22, 2009 kwa barua iliyotiwa saini na Kamishna wa Madini, wakati huo, Dk. Dalaly P. Kafumu baada ya wamiliki hao wapya wa leseni hiyo kulipia malipo ya uhamisho ya Dola za Kimarekani 200.

Hata hivyo, utata wa uhalali wa kampuni hiyo kuruhusiwa kuchimba dhahabu ndani ya mito hiyo ulijidhihirisha kwenye andiko la tathmini ya athari ya uharibifu wa mazingira kuhusu mradi huo (Environmental Impact Assessment - EIA), ambapo ilionyesha Wachina wale kutumia idhinisho la EIA iliyotayarishwa na KAMAKA CO. LIMITED ambao ni wamiliki wa awali wa leseni hiyo kabla haijahamishiwa kwa kampuni hiyo ya Kichina. Waraka huo haukuonyesha iwapo ulipitiwa upya na Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC).

---
Makala hii ya Felix Mwakyembe kupitia gazeti la Raia Mwema