Watozwa 6,000/= kwa kujifungulia majumbani

WAUGUZI wa Zahanati ya Izava, iliyopo Kata ya Segala, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wamelalamikiwa kwa kitendo cha kuwatoza sh 6,000 kwa kila mzazi anayejifungulia nyumbani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumapili, wajawazito hao walisema kuwa wauguzi wa zahanati hiyo wamekuwa na tabia ya kuwatoza fedha hizo wanapojifungua nyumbani na kuwapeleka watoto hospitalini.

Mmoja wa wajawazito hao, Mwanaidi Bakari, alisema miongoni mwa sababu zinazowafanya
wajifungulie nyumbani ni wauguzi hao kuwataka waende zahanati wakiwa na wakunga wao wa jadi ili wawasaidie.

Alisema kutokana na hali hiyo, wajawazito waliamua kujifungua nyumbani kwa kuona kwamba wauguzi wenye taaluma wanashindwa kuwasaidia bila kuwategemea wakunga.
“Tunashangaa, kwa kitendo hicho wengi wetu tumeamua kujifungulia nyumbani na wakunga wa jadi, lakini cha ajabu tunatozwa kiasi cha fedha sh. 6,000,” 
alisema Mwanaidi.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, James Charles, alisema si utaratibu wa serikali kutoza fedha hizo na kueleza kuwa ni kinyume na taratibu na kuwataka wananchi kutoa taarifa ili hatua za kisheria zifuatwe.
“Hatuwezi kuvumilia kitendo hicho, wanalipwa mishahara na serikali kwa ajili ya kuwahudumia wanajamii pindi wanapohitaji huduma za kiafya,” 
alisema Charles.