Zanzibar: Wizara yachukulia hatua madai ya wanafunzi kufundishwa Biblia

SAKATA la Skuli ya Eden International School iliyopo Shakani imechukua sura mpya baada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu Zanzibar kulifatilia kwa kina na kujua elimu inayotolewa skulini hapo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mrajis wa Elimu kupata taarifa kupitia vyombo vya habari ikiwemo kuchapishwa habari hiyo katika gazeti la Zanzibar leo juu ya malalamiko hayo kutoka kwa wazazi wanaosoma skuli hiyo.

Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari Mrajis wa Elimu Siajabu Suleiman Pandu, huko Ofisi kwake Majestik alisema ni kweli mmiliki wa skuli hiyo amekuwa akitoa elimu ya Bibilia kwa wanafunzi wa msingi.

Aidha alisema baada ya kufanya uchunguzi katika skuli hiyo alibaini vipande vya aya ambavyo vilibandikwa katika baadhi ya madarasa huku vivazi vya wanafunzi vikiwa haviridhishi kulinganisha na Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Mrajis Siajabu alifahamisha kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kila mtu ana haki ya kuabudu dini yake na ndio maana Wazanzibari wanaishi kwa amani na utulivu wa hali ya juu.

Alisema kwa mujibu wa katiba hiyo hakuna kosa mtu kufundisha dini, bali ni kosa kuwalazimisha watoto kusoma dini ambayo sio ya kwao jambo ambalo limewasikitisha wanafunzi wa skuli hiyo kukosa kusomeshwa dini ya Kiislam.

Hata hivyo alisema uchunguzi wake pia umebaini kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ni waislam.

“Wakati nilipokuwa nikipata maelezo kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa kiislamu wanaosoma katika skuli hiyo walisikitishwa sana kutosomeshwa dini yao huku wakiwa wengi wao ni waislamu.

Alisema sheria ya elimu kifungu 47 hadi 48 kinasema kuwa skuli au tasisi za kidni zinaweza kuanzishwa chini ya sheria hiyo kifungu kidogo (2) pale skuli au tasisi za aina hii zinapoanzishwa masharti ya kifungu cha 13 cha sheria hii yatatumika ipasavyo na (3) kwa madhumuni ya sehemu hii skuli au tasisi za kidini hazitojumuisha darasa au mafundisho mengine ya kidini yanayotolewa misikitini, makanisani au katika sehemu nyengine zozote za ibada mradi tu darasa au mafundisho hayo ni ya kidini kwa kila hali.

Hata hivyo alifahamisha kuwa kifungu 48 kinasema kuwa bila ya kujali masharti ya kifungu cha 47 cha sheria hii mafundisho ya kidini yataweza kutolewa katika skuli yoyote ya Serikali au binafsi au inayosaidiwa mradi wakati utekelezaji wa masharti ya kifungu hiki imani za kidini mbalimbali walizomo wanafunzi zitazingatiwa ili kuhakikisha kwamba mwanafunzi anapatiwa mafundisho ya dini ile inayomruhusu.

Alisema Mmiliki huyo ambae ni Pilsoon Youn maarufu (Mama Kim) wamekuja hapa Zanzibar kama ni shirika Afrika Agape Assosiation kwa ajili ya kuanzisha skuli na kusomesha watu masuala ya kidini na kumjua mungu.
“Wakati walipofanya kikao na wazazi wa watoto hao akilanusha kusomesha dini ya aina yoyote.”

Sambamba na hayo alisema kama Wizara tayari imeshajipanga na kuandika ripoti ili hatua nyengine za kisheria zichukuliwe.

“Sisi kama Wizara tayari tumeshajipanga na tunaendelea kujipanga kulifanyia kazi suala hili kwa kuliandikia ripoti ili hatua nyengine zichukuliwe kwani kama Mrajis sina mamlaka ya kuifungia skuli hii bali wenye mamlaka ni Baraza la elimu,” alifafanua Mrajis Siajabu.

Akizungumzia kuhusu usajili halali wa skuli hiyo alisema kwa mujibu wa taarifa aliyoipata ZIPA usajili wa skuli hiyo sio wa kudumu ambao ilisajiliwa kwa namba RPS/329 mwaka 2010/2011.

Chanzo cha habari: Gazeti la Zanzibar Leo, wavuti.com imeinukuu kutoka ZanzibariYetu blog