Aeleza walivyotapeliwa milioni 29/= na 'mganga Manyaunyau'

Shahidi wa pili katika kesi ya kujipatia Sh29.6 milioni kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mganga wa jadi, Dunia Salumu (37) ‘Manyaunyau’ amedai kuwa walilazimika kuuza kiwanja na nyumba ya urithi kutafuta fedha za kununua mabeberu saba na mafuta ya ngamia ili kumpa mganga huyo kama masharti ya kumfufua ndugu yao aliyefariki dunia.

Manyaunyau alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Desemba mwaka 2013 akikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha hizo kutoka kwa Tecla Modest.

Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Nassoro Katuda shahidi huyo, Diana Steven (26) alidai kuwa baada ya kumaliza matanga ya mjomba wake, Saimon Modest aliyefariki mwaka 2008, wakiwa
nyumbani Mchikichini, Dar es Salaam walisikia sauti ya mtu ikisema kuwa ‘mimi sijafa’.

Wakati Diana akiendelea kutoa ushahidi huo mrefu, Hakimu Wilberforce Luhwago, alimkatisha akieleza kuwa ameisikiliza kesi hiyo kwa muda mrefu na kuna nyingine za kusikiliza, hivyo itaendelea Agosti 13, mwaka huu.

Alisema siku tatu baada ya mazishi ya mjomba wake, ndugu yao aitwaye Hamisi akiwa na Manyaunyau walifika nyumbani kutoa pole na walipofika Manyaunyau alidai kuwa marehemu hajafa, bali ameuawa na kaka yake na amechukuliwa na Mpemba kwa ajili ya kwenda kuuza duka.

“Mimi na mama zangu wawili tulishtushwa na kuhoji, mtu aliyekufa anaweza akawa hai?” alisema Diana katika ushahidi wake uliochukua saa nane.

“Baada ya hapo alituambia siku iliyofuata twende ofisini kwake (Manyaunyau), Mburahati, tukiwa na Sh100,000. Mama zangu walisema hawana, lakini ndugu yetu mmoja aitwaye Bright Steven alikwenda kwenye ATM na kuchukua Sh80,000 na safari ikafanikiwa,” alidai.

Diana alisema baada ya kupeleka fedha hizo, Manyaunyau aliwapangia kwenda siku nyingine, akiwataka kurudi wakiwa na kitambaa cheusi na walipokipeleka alisema alikichukua na kukifunika kikaanza kutoa sauti ya mtu mzima ikisema: “Karibuni sana wajukuu zangu na maelezo yote mtapewa na mwenyeji wenu.”

Alisema Manyaunyau pia aliwataka wapeleke chupa sita za mafuta ya ngamia wakiyakosa wampelekee Sh1.8 milioni. Alisema walimpelekea fedha hizo walizozipata kwa kuuza sehemu ya kiwanja walichorithi kwa mama yao.

“Siku tuliyopeleka hiyo hela pia tulipeleka mtama, jogoo mwekundu na tulipelekwa katika pori lililopo Kibamba na kila tulipokuwa tukienda kule Kibamba tulikuwa tunakodi teksi kwa Sh40,000,” alidai Diana.

via Mwananchi