Ajira zilizolalamikiwa kutolewa kiupendeleo zimefutwa

Hatimaye zile lawama kuhusu upendeleo wa ajira katika Idara ya Uhamiaji kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, zimefutwa baada ya Kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo kubaini kuwa ni kweli nafasi hizo ziligawiwa kwa upendeleo bila ya kufuata taratibu, kanuni na sheria za ajira.

Ajira hizo zilitangazwa Februari 17, mwaka huu na watu 15,707 walijitokeza kuwania nafasi hizo 200, miongoni mwao, waombaji 1,005 waliitwa kwenye usaili na waliothibitishwa waliitwa kazini.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye ndiye aliyeiongoza Kamati hiyo, Mbarak Abdulwakil amesema nafasi hizo zitatangazwa upya na kusimamiwa na Wizara hiyo badala ya Idara husika.
“Kamati hiyo iliyoanza kazi yake Agosti Mosi, mwaka huu ilibaini kwamba hata kigezo cha umri, ambacho ni miaka 25 kwa konstebo na miaka 30 kwa koplo hakikuzingatiwa kwani wenye umri zaidi ya huo waliitwa kazini... “Lakini zaidi, baadhi ya wasailiwa walioitwa kazini ni ndugu na jamaa wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji.”
Aidha, ajira hizo zilizofutwa zinahusisha pia nafasi 28 zilizokuwa zimetangazwa kupitia Idara ya Uhamiaji Zanzibar.

Ilitanabahishwa kuwa si kosa kwa ndugu na jamaa wa watumishi kuajiriwa iwapo wanakidhi vigezo vyote, lakini inapotokea kwamba hakuna msimamizi huru ni wazi kwamba kunakuwa na upendeleo kama ilivyotokea.