Albino 20 wapewa simu na Kamanda Kova na SAPNA Electronics

Kamishna wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova akimkabidhi Mwenyekiti wa chama cha albino Dar es Salaam, simu kwa ajili ya albino waishio jijini Dar es salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewashauri albino wanaoishi jijini humo kuwa karibu sana na jeshi hilo ili kurahisisha mawasiliano kati yao na Wakuu wa vituo vya Polisi vilivyo karibu na makazi yao au wanapofanyia usalama wao jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa Polisi wa Kanda hiyo Maalum ya Polisi, Suleman Kova amewataka kwa sasa waongeze mawasiliano na jeshi la Polisi kutokana na taarifa za uhalifu dhidi ya albino katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
 
Kova ameongea na albino hao ofisini kwake kuwataarifu kwa ujumla kuhusu jitihada kubwa sana za
jeshi hilo za kupambana na maadui wa albino ambao wengi wao wameshakamatwa na kufikishwa mahakamani na baadhi yao kuhukumiwa.

Katika kufanikisha zoezi hilo la mawasiliano ya haraka na Jeshi la Polisi, Kamishna wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau kampuni ya SAPNA ELECTRONIC ametoa simu 20 kwa albino ambao wameudhuria kikao ili iwe rahisi kwao kuwasiliana Jeshi la Polisi kwa namba 0787-668306 ambayo ipo katika chumba cha dharura katika Kikosi cha 999.

Kamishna Kova anahimiza wadau mbalimbali  watoe misaada zaidi kwa albino ili waweze kupata simu za mikononi, mafuta maalum ya kupaka ngozi zao na misaada mingineyo kupitia kwa namba 0715 – 009983 (namba ya Kamishna Kova ya ofisi) au 0756-710179 ambayo ni ya Msaidizi wake, SP. MOSES NECKEMIAH FUNDI.

Kamanda Kova amesema hatua nyingine za ziada za muda mfupi na mrefu za kuwasaidia albino ni programu ya mafunzo maalum kwa albino wa jijini Dar es Salaam ili wapate mafunzo kupitia dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kwa lengo la kupata uelewa wa kutosha ili washiriki na kujua namna ya kutoa taarifa kwa lengo la kujikinga na maadui wao.