MANSOUR Yusuf Himid (47) ndiyo habari kuu ya Zanzibar hivi sasa. Hata hivyo, miaka miwili iliyopita, hali ilikuwa tofauti baada ya kutolewa kwa ripoti ya Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi kuhusu masuala ya ardhi.
Kamati hiyo ilibaini ufisadi mkubwa katika sekta ya ardhi Visiwani humo, huku jina la Himid pamoja na familia ya rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume, vikiwa vimetanda.
Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo teule ilibaini kwamba wakati Himid akiwa Waziri wa Ardhi, familia ya Karume ilipata ardhi katika maeneo nyeti pasipo kufuata sheria.
“Kumekuwapo uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira kwenye hoteli inayopakana na Chuo cha
Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Maruhubi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani-Zanzibar na Hoteli ya Misali iliyopo Wesha, Chake Chake-Pemba.
“Kamati imejiridhisha kwamba Ramadhan Abdallah Songa na Mama Fatma Karume walishiriki katika udanganyifu wa mkataba wa mauziano uliofungwa baina ya Serikali na Kidawa.
"Aidha, hati ya matumizi ya ardhi aliyopewa Karume na Mansour Yussuf Himid, (Akiwa Waziri wa Ujenzi, Nishati na Ardhi), imekiuka taratibu za kisheria na kiutawala)," imeandika sehemu ya ripoti hiyo iliyosomwa katika Baraza la Wawakilishi na Mjumbe wa Baraza hilo, Omar Ali Shehe.
Kidawa linasimama badala ya jina la Juma Hamad Kidawa ambaye alifanya biashara hiyo ya mauziano ya ardhi ya Amina Karume (mtoto wa hayati Karume) pasipo kufuata sheria za nchi.
Himid ni shemeji wa Karume kwa maana mbili. Wote wameoleana.
Miaka nane kabla, Himid alikuwa sehemu ya mashambulizi ya kalamu kali ya Ali Nabwa (sasa marehemu), kupitia gazeti lililopigwa marufuku Visiwani Zanzibar laDIRA, lililokuwa likieleza namna uhusiano baina ya familia ya Karume na Himid unavyochochea ufisadi Visiwani humo.
Gazeti la DIRA lilikuwa kipenzi cha wanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF) na viongozi wa chama hicho walilitumia kuvurumisha mashambulizi yao kwa Himid.
Lakini, mwaka mmoja baada ya Himid kufukuzwa kutoka ndani ya CCM na hivyo kupoteza nafasi yake ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Jimbo la Kiembesamaki, mwanasiasa huyo anatajwa kama shujaa na Wazanzibari.
Katika ukurasa wake binafsi wa facebook wiki iliyopita, Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe kupitia CUF, Ismail Jussa Ladhu aliandika;
“Sasa ni wajibu wetu Wazanzibari kujipanga vyema na kutoyumbishwa na majaribio haya yanayoendelea yakiwa na lengo la kutaka kututia katika misukosuko ili tusishughulikie lengo kuu la mabadiliko 2015.
“Haturudi nyuma na kwa pamoja tutaleta mabadiliko mwakani chini ya mashujaa Maalim Seif Sharif Hamad na Mansoor Yussuf Himid. We Can! Yes, We Can.”
Himidi alikamatwa wiki mbili zilizopita na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya short gun yenye risasi 112 na bastola yenye risasi 295 kinyume cha sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Naibu Msaidizi Mkuu wa Upelelezi Zanzibar, Salum Msangi, kisheria, mtu anaruhusiwa kumiliki risasi 50 za short gun na risasi za bastola zinatakiwa kuwa 25.
Nguvu ya Mansour
Zaidi ya ushemeji wake na Karume, Mansour ana nguvu Visiwani Zanzibar kwa sababu ni mtoto wa Brigedia Jenerali, Yusuf Himid, ambaye alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Vikosi vya SMZ baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Hivyo, kuwa Mansour na Amani Karume wameoleana kunakutanisha familia mbili ambazo zimehusika na Mapinduzi ya Zanzibar “kindakindaki.”
Mmoja wa mawaziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ameliambia Raia Mwema wiki hii kwamba Himid na Amani Karume wana utajiri mkubwa na ushawishi katika siasa za Wazanzibar na kwamba muunganiko wao na CUF ni hatari kwa CCM.
“Hizi jitihada unazoona za CUF kumkumbatia Himid zina maana yake. Wanajua mapungufu yake lakini wanafahamu kwamba kwa kumpata yeye na Karume, watakuwa wamefanikiwa kuvunja sehemu ya ngome ya CCM.
“Mansour na Karume wana pesa. Wanaifahamu CCM kindakindaki. Wanayafahamu Mapinduzi ya mwaka 1964 kindakindaki. Huwezi ukasimama mbele ya wafuasi wao na kusema wao hawayatambui Mapinduzi ya mwaka 1964.
“Hii ndiyo ilikuwa kete ya CCM kwa CUF kila wakati wa uchaguzi na sasa hawataweza kuitumia dhidi ya mahasimu. Akina Maalim Seif wanaweza kugeuka baadaye lakini si kabla kwanza hawajapata madaraka Zanzibar,” kilisema chanzo hicho ambacho kwa sasa kimekataa kutajwa jina lake.
Mansoor pia ana hazina miongoni mwa baadhi ya waasisi wa mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, waliofanya kazi na baba yake kwa karibu sana.
Ndiyo maana, yeye ni miongoni mwa wajumbe wa kamati inayofahamika kwa jina la Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar –Inayoundwa na watu sita; wakiwamo wanachama watatu maarufu wa CCM na wengine watatu wa CUF, chini ya Hassan Nassor Moyo.
Karume na CUF
Mwanzoni mwa mwaka huu, gazeti hili liliambiwa na mojawapo ya vyanzo vyake kwamba Karume aliamua kujiweka karibu na CUF kwa vile aliona hana nguvu kubwa za kisiasa Visiwani Zanzibar.
“Unajua wakati anawania urais wa Zanzibar mwaka 2000, Karume hakuwa na nguvu yoyote ya kisiasa pale Zanzibar. Hata Dk. Mohamed Ghalib Bilal, alikuwa na nguvu kumzidi. Alipata urais kwa sababu tu watu wa Bara walimtaka.
“Baada ya kuona kwamba hana nguvu sana Zanzibar miongoni mwa wahafidhina, Karume ameamua kuunganisha nguvu na wenzetu wa CUF, jambo linalompa nguvu kwa wananchi lakini linampa shida serikalini,” kilisema chanzo hicho.
Watafiti wa siasa za Zanzibar wanakubaliana kwamba Mansoor hana nguvu za kisiasa kama walizokuwa nazo Seif Shariff Hamad na Aboud Jumbe Mwinyi wakati walipovuliwa nyadhifa zao za kisiasa, lakini nguvu yake kubwa iko katika maelewano aliyofanya na Karume na watu wa CUF.
Karume amekuwa karibu na siasa za CUF kutokana na kufanikisha kwake maridhiano ya sasa ya Zanzibar, baada ya kukutana na Maalim Seif kwa siri.
--