Amkata mwanaye kutengeneza njia ya kutolea haja kubwa
Wiki iliyopita mkazi wa Kata ya Kitangiri katika Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, Anastazia Ngilitu, alimchanja kwa wembe mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili baada ya kuzaliwa bila kuwa na njia ya kutolea ya haja kubwa.

Taarifa zinasema Mama huyo ambaye ni mkazi wa mkoani Tabora, wakati wa kujifungua mtoto huyo, alijifungulia watoto mapacha watatu (njiani) kwenye mtaro wa maji uliopo katika eneo analoishi kwa sasa kisha yeye pamoja na watoto wake walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu ambapo watoto wawili walikufa baada ya kufikishwa Hospitalini na kubaki na mtoto mmoja mwenye tatizo hilo.

Anastazia amesema aliafanya hivyo kutokana na kukosa fedha za kumtibu mwanaye kujaa tumbo na kumfanya alie kwa muda mrefu.

Amesema alipojifungua, mtoto huyo alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Bugando lakini baada ya muda mfupi hali hiyo ilijirudia ndipo alipoamua kumnasua kwa kumchana.