![]() |
Hali halisi. Pichani Darasa la awali katika shule ya msingi Sima B katika halmashauri ya mji wa Bariadi mkoa wa Simiyu likiendelea. |
SERIKALI imelaumiwa kwa kushindwa kuwekeza rasilimali za kutosha katika utoaji wa Elimu ya Awali kama inavyoelekezwa na Mtaala wa utoaji wa elimu hiyo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa juzi na Wadau wa Elimu mjini Bariadi wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika maeneo tofauti juu ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu hasa utoaji wa Elimu ya awali.
Walisema kuwa licha ya jamii kuwa na ufahamu wa elimu hiyo lakini Serikali bado haijawa na nia ya
dhati kwa kuelekeza raslimali za kutosha za kuwezesha kutolewa kwa kiwango kinachokubaliwa kama ilivyoelekezwa na Mtaala wa Elimu ya awali.
“Jamii kwa sasa imekuwa na uelewa mkubwa sana juu ya Elimu ya awali ndiyo maana ukitembelea madarasa hayo yana wanafunzi wengi kuliko uwezo wake lakini jambo la kusikitisha serikali bado haijaona umuhimu wa kuwekeza ndiyo maana elimu hii katika mazingira yaliyo mengi ni ya kusikitisha”Alisema Rose John.
Walisema kuwa utoaji wa elimu hiyo wilayani humo umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja ukosefu wa vyumba vya madarasa ya kusomea wanafunzi huku wengine wakisomea chini ya mti na hata shule zenye madarasa hayana mahitaji muhimu kwa ajili wanafunzi hao.
![]() |
Darasa linaendelea |
Naye Mwalimu, Yunice Mahega anayefundisha darasa la awali katika shule ya Msingi Sima ‘A’ mjini humo anasema kuwa wana darasa moja la elimu ya Awali lakini mazingira yake si rafiki kwani kimsingi elimu hiyo inatakiwa kutolewa katika mazingira maalum tofauti na ilivyo kwa vyumba vya shule za kawaida.
“Chumba cha kufundishia elimu ya Awali kinapaswa kuwa tofauti na vyumba hivi vingine ona hapa kwetu hiki chumba kinapaswa kutumiwa na wanafunzi wakubwa na si hawa watoto pia yanapaswa kuwa na madawati ambayo ni mafupi ili yakidhi vimo vya wanafunzi lakini siye unaona hatuna hata dawati moja watoto wanakaa chini”,anasema Mwalimu Mahega kwa uchungu.
Aliongeza a kuwa licha ya kufuata Mtaala katika kufundishia elimu hiyo lakini idadi kubwa ya wanafunzi darasani ni mojawapo ya tatizo kwani Mtaala unaelekeza uwiano ni chumba kimoja kwa wanafunzi 25 wakati katika shule hiyo kuna wanafunzi 90.
Akizungumzia hali hiyo Ofisa Elimu Shule za Msingi wa Mji wa Bariadi,Samwel Muyemba anakiri kuwepo kwa hali hiyo huku akisisitiza ya kuwa idara yake inajitahidi kukabiliana na changamoto hizo kadri wanavyopata pesa kutoka serikalini.
Alisema kuwa miundo mbinu si rafiki kuwezesha elimu hiyo kutolewa kulingana na inavyoelekezwa na Mtaala huku akitolea mfano kuwa shule zilizo nyingi katika halmashauri hiyo hazina vifaa kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia na kufundishia pamoja na michezo.
Samwel Mwanga
Simiyu
via Malunde1 blog