Barua ya wazi ya Ally Saleh kwa Rais Kikwete

KUHUSU: MADAI YA KUTESWA MAHABUSU WANAOTUHUMIWA KWA MAKOSA YA UGAIDI


Ndugu Rais,

Nisamehe sana nakuandikia barua ya wazi, lakini mimi raia wako sijui njia nyepesi ya kuweza kukufikishia waraka huu, maana sizijui taratibu zilizotandikwa na za wazi za kufanya hivyo.

Mheshimiwa Rais, waraka huu unahusu madai ambayo wiki mbili hizi yamekuwa yakiandikwa katika vyombo vya habari kuhusiana na watu kadhaa ambao wako mahabusu kukabili makosa ya ugaidi.

Mimi ni katika raia wako wanaopenda mfumo wa sheria ufanye kazi, na ndio maana barua hii si kulalamikia
kushtakiwa kwa watu kadhaa kwa wakiwemo wengi kutoka Zanzibar kwa makosa ya kigaidi.

Vitendo vya kigaidi havikubaliki na kwa hakika havichagui wala havibagui na yeyote mwenye kuvifanya, kuviendeleza au kusaidia ni lazima akabili sheria.

Mheshimiwa Rais, najua una wajibu wa kulinda usalama wa nchi ikiwa ni pamoja na raia na mali zao na kwa hivyo wewe ndie muangalizi mkuu wa sheria za nchi na kuona haki
inapatikana kwa kila raia. Lakini katika kusimamia huko kila mtu atashtakiwa na kukabili kesi yake kwa kiwango cha juu cha heshima na pia kupewa haki ya kuyajua na kujitetea kwa mashtaka ambayo atakuwa anakabiliana nayo.

Nchi yetu ina vyombo kadhaa vya usimamizi wa haki kama ambavyo kuna vyombo kadhaa
vya ulinzi wa haki zetu na vyote kwa mujibu wa Katiba yetu viko chini yako wewe.

Mheshimiwa Rais, naamini sina haja ya kunukuu vifungu vya haki za binaadamu ambavyo vinampa mfungwa haki hizo na hata kama itathibitika kosa lake bado chini ya Katiba yetu mfungwa hapaswi kufanyishwa kazi za kutwezwa na za kitumwa.

Naamini kabisa unajua kuwa kumekuwa kuna madai ambayo yametoka kwenye vyombo vya habari yanayowahusu washtakiwa katika kesi ya ugaidi ambayo ipo Mahakamani mjini Dar es Salaam hivi sasa.

Washtakiwa hao wamesema Mahakamani kuwa wanateswa kwa njia ya kupigwa, wanafanyiwa vitendo vya kinyama kama vile kutiwa chupa na majiti sehemu zao za siri. Pia wamedai kuwa hawapati matibabu.

Kwa kuwa madai hayo yametolewa Mahakamani, niruhusu Mheshimiwa niseme kwamba hayawezi kabisa kupuuzwa na itakuwa ni kosa kubwa kwako kuyapuuza.

Ingekuwa vitendo hivyo ni sehemu ya mfumo wa upatikanaji haki, nisingekuwa na sababu ya kuandika barua hii, lakini kwa sababu vitendo hivyo ni uvunjaji wa haki ya watu waliozuliwa na pia ni uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu, ndio imenilazimu kukuandikia.

Wananchi wako na dunia nzima wanafuatilia juu ya kesi hii. Na habari tunazopata ni hizo za maafisa wetu wa kutulinda kujihusisha na matendo kama hayo kwa watu ambao wana
heshima kubwa katika jamii. Haya tumekuwa tukiyasikia kwengine lakini sasa yapo kwetu.

Leo wapo Mahakamani wanakabili shitaka na kesho wanaweza kuwa wapo nje kwa
kutoonekana hawana kosa, jee heshima yao kwa kudaiwa kufanyiwa vitendo kama hivyo
itakuwa wapi mbele ya macho ya umma?

Lakini mfumo wetu wa sheria Mheshimiwa Rais unaelekea kufikia kiasi cha kuzama kama hivyo? Hivi inastahili kufanyiana kama hivyo?

Nchi yako Mheshimiwa Rais ni mwanachama wa Jumuia zote za kusimamia haki za binaadamu baada ya kutia saini na kuridhia mikataba yote katika eneo hilo, jee huku ndio
kutimiza wajibu wetu? Huku ndio kujenga imani kuwa haki za binaadamu na haki za
wafungwa zinalindwa?

Kwa fikra zangu Mheshimiwa Rais hili si neno la kupuuzwa. Haya yamelalamikiwa hadharani na washtakiwa lakini wasaidizi wako wote hayajatoa kauli yoyote ile. Si Mkuu wa Polisi, si Mkuu wa Idara ya Usalama, si Mkuu wa Idara ya Magereza.

Pia wasaidizi wako Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheri Mkuu, Muendesha Mashtaka
walipaswa kutoa kauli juu ya kinachoendelea katika magereza dhidi ya washtakiwa hao kwa kuwa kimelalamikiwa Mahakamani na kwa hivyo kipo hadharani na mbele ya macho ya umma.

Kwa kuwa madai ya kuteswa na kudhalilishwa ni makubwa ni ushauri wangu Mheshimiwa Rais kuona kuwa unachukua hatua ya kuchunguzwa matendo hayo halan, yaani kwa Kiswahili cha kwetu ni kwa haraka inavyowezekana.

Naamini utakuwa na njia zako za kuchukua kwa kufanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa hatua, ila, la kwangu lilikuwa ni kukuarifu kama ulikuwa hujui, kukuzindua kama ilikuwa umeghafilika na kubwa zaidi ni kulisema ili kesho na kesho kutwa iwe angagalau sauti moja ilinyanyuka kueleza juu ya madhila hayo.

Khofu yangu jambo hili lisipochukuliwa hatua kwa kuchunguzwa na wahusika kuadhibiwa ina maana itakuwa tunalilea, na mbali ya kukosa heshima kwa macho ya kimataifa, basi pia itakuwa ni dua kubwa kwa Serikali.

Naomba tena unisamehe Rais wangu lakini roho yangu haingeweza kabisa kulistahamilia
hili. Kama ilivyotokea huko Urusi ya Kikomunisti kulikozuka msemo kuwa usipolisema la mwenzio hakutakuwa na wa kukusema likufikapo wewe.

Ally Saleh
Zanzibar