BMK: Wajumbe waridhia madaraka ya Rais kupunguzwa

BAADHI ya wajumbe wa kamati namba 12, wamekubaliana kupunguza majukumu ya Rais na kutengwa kwa orodha ya viongozi ambao Rais anaweza kuwateua endapo atafanya uteuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Paul Kimiti, alisema kamati yake pia imeridhia utaratibu wa uraia pacha.

Kimiti alisema wajumbe wa kamati yake wameona wapunguze majukumu ya Rais, ikiwa ni pamoja na kumtengea orodha ya viongozi, ambao anaweza kuwateua wakati akifanya uteuzi.

Alisema mbali ya orodha hiyo, mamlaka nyingine zitaendelea na utaratibu wake, ikiwemo Tume zitakazoundwa.

Kimiti alisema wajumbe hao walisisitiza kwamba Rais atakapokuwa anateua viongozi, ni vizuri wathibitishwe na wabunge ili bunge liwe na uhakika na uteuzi huo.

“Ukifanya makosa katika suala la uongozi, utakuwa umeangamiza nchi yako na ndiyo maana tumesema tutalisimamia vizuri mpaka tufikie muafaka, na muafaka utakaofikiwa tutaupeleka kwenye Bunge Maalumu ili ukajadiliwe,’’ alisema.

via gazeti la Uhuru, Dodoma