Brigedia Hashim Mbita atunukiwa na Rais Mugabe Tuzo ya Juu ya Taifa la Zimbabwe "Royal Order Of Mwanamutapa" US$100,000

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe akimkabidhi Bi. Sheila Hashim Mbita, binti yake Brigedia Jenerali Mstaafu Hashim Mbita, Tuzo ya Juu ya Taifa la Zimbabwe ya Nishani ya Royal Order Of Mwanamutapa kwa kutambua mchango wake katika ukombozi wa Taifa la Zimbabwe na nchi nyingine kusini mwa Afrika. Rais Mugabe alikabidhi tuzo hiyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe. (picha: Fred Maro)

Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeishukuru na kuipongeza tena Tanzania kwa mchango wake mkubwa na wa hali na mali uliofanikisha jitihada za mapambano ya ukombozi yaliyoleta uhuru kwa nchi za Kusini mwa Afrika.

Aidha, SADC imemshukuru na kumpongeza aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika, Brigedia Hashim Mbita wa Tanzania, kwa mchango wake na uongozi wake wa mapambano ya
ukombozi, iwe katika nyanja ya kuviwezesha vyama vya ukombozi kwa hali na mali, raslimali na ushauri.

Pongezi hizo kwa Tanzania zilitolewa usiku wa jana, Jumamosi, Agosti 16, 2014, na Kikao cha Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC – SADC Troika- kilichofanyika kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe, chini ya Uenyekiti wa Rais Hifikepunye Phohaba wa Namibia.

Mkutano huo wa SADC Troika ulihudhuriwa na wanachama wa Asasi hiyo – nchi za Namibia, Lesotho na Tanzania. Nchi za Afrika Kusini, Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilishiriki kama waalikwa maalum wa kikao hicho.

Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya nwenzake, Rais Pohamba alisema: “Tunawashukuru wananchi wa Tanzania kwa mchango wao wa kiuchumi, kijeshi na kimkakati katika kuunga mkono kwa hali na mali jitihada za mapambano ya ukombozi wa nchi zetu.”

Aliongeza Rais Pohamba: “Sote tunaijua Tanzania, sote tunawajua Watanzania. Kwa pamoja walitoa jasho na damu na sisi wenyewe katika kutafuta ukombozi wa nchi zetu. Tutaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wao mkubwa na usiosahaulika kwa ustawi wa nchi zetu.”

Kuhusu Mzee Mbita, ambaye Ripoti yake ya shughuli za ukombozi ilitarajiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC, Rais Pohamba alisema: “Brigedia Mbita alifanya kazi mchana na usiku kufanikisha shughuli za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Tunamshukuru sana kwa uongozi wake na mchango wake mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi zetu.”

Aliongeza: “Brigedia Mbita ni raia wa Tanzania na alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyokuwa na makao makuu yake mjini Dar es Salaam. Alichapa kazi kweli kweli na chini ya uongozi wake, vyama vya ukombozi vilipata misaada ya hali na mali, misaada ya kiroho na ushauri wa kijeshi kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa mtu wa shughuli za jeshi.” Mzee Mbita aliongoza Kamati ya Ukombozi tokea mwaka 1974 hadi ilipomaliza shughuli zake.

Akizungumza kwa ufupi sana katika kikao hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimpongeza sana Brigedia Mbita akisema kuwa alifanya kazi nzuri na kubwa na “tunampogeza kwa kazi nzuri sana ya kuandaa Ripoti hiyo.”

Ripoti hiyo inayojulikana kama Mradi wa Hashim Mbita iliongozwa na Meneja wa Mradi, Profesa Arnold Temu wa Tanzania na imechapishwa na Kampuni ya Mkuki na Nyota, pia ya Tanzania, ambayo Mtendaji Mkuu wake, Mzee Walter Bgoya ameandamana na mwakilishi wa Mzee Mbita kwenye mkutano huo.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

17 Agosti,2014