Chahali aamua "kuchukua hatua za vitendo dhidi ya unyanyasaji mtandaoni"

Nadhani wengi wenu wasomaji mnafahamu kilichomsibu Betty Ndejembi, aliyetutoka juzi. Kabla ya kufariki kwake aliandamwa na unyanyasaji wa kutosha katika mtandao huo. Baada ya kifo hicho, mie niliungana na 'wenye mapenzi mema kwa jamii' kukemea unyanyasaji mtandaoni, kwa kimombo 'cyberbullying.'

Hata hivyo, katika kuhamasisha mapambano hayo sikumtaja wala kumtuhumu mtu kuwa ni mnyanyasaji wa wenzie mtandaoni. Nilichohamasisha ndicho hicho nilichoeleza hapo juu: sie watumiaji wa mtandao kama wahanga wa unyanyasaji wa mtandaoni kuunganisha nguvu zetu dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo. Na kwa hakika mapokeo yamekuwa mazuri sana. Watu wengi wamewasiliana nami kunifahamisha jinsi walivyokuwa wahanga wa cyberbullying.

Wito wangu kwa jamii umekuwa sio kusubiri serikali au wanasiasa kuchukua hatua ya kukomesha tabia hiyo bali sie kama wananchi na wahanga wa tabia hiyo kuunganisha kuvu na kupambana nayo. Kwa lugha nyingine, sie wenyewe tuchukue uongozi wa mapambano dhidi ya wanyanyasaji wa mtandaoni.

Hata hivyo, jioni ya leo likaibuka kundi la watu waliaonza kunishambulia vikali kuhusiana na kampeni hiyo ya kupambana na unyanyasaji mtandaoni. Kikubwa ni tuhuma kwamba mie wanayeniita 'mwanaharakati wa
cyberbullying' ni 'bully' (mnyanyasaji) pia. Na mmoja wao akapata ujasiri wa kupitia tweets zangu za nyuma na kuzi-screenshot ili 'kuthibitisha kuwa mie ni mnafiki nisyestahili kukemea cyberbullying.' Wakati mwingine huwa nashangazwa na 'ujasiri' wa aina hii ambao hata kwa mwenye uelewa mdogo tu wa sheria anaweza kujua athari zake.

Hadi hapo sikuona tatizo sana japo nilishangazwa na 'hasira' za watu hao ilhali sikuwahi kuwatuhumu kuwa wao ni bullies. Na hata asubuhi nilitwiti kuhoji ''kama tunapozungumzia ufisadi, hukasiriki kwa vile wewe si fisadi, kwanini tukizungumzia cyberbullying ukasirike ilhali wewe sio cyberbully?"

Lakini katika mwendelezo wa shutuma zao dhidi yangu, mmoja wao akavuka mstari wa kisheria. Siwezi kuliongelea kiundani suala hili kwa sababu za kisheria.

Awali nilipoamua kuungana na wengine kukemea unyanyasaji mtandaoni sikudhani kwamba itafika mahala pa kuchukua vitendo kulazimisha wanyanyasaji hao waache tabia hiyo. Hata hivyo, kwa kilichotokea leo, nimeamua kuhamia kwenye vitendo.

Tuna tatizo kama Watanzania, ni wepesi wa kulalamikia matatizo yanayotukabili lakini ni wagumu kuchukua hatua za vitendo kuyatatua. Mgao wa umeme, huduma mbovu za baadhi ya makampuni, tatizo la ajali zisizoisha, ufisadi, na kadhalika. Kwa kiasi kikubwa tumekuwa watu wa kulalamika tu kana kwamba malalamiko hayo yataleta mabadiliko.
Katika hili la unyanyasaji mtandaoni, asilimia kubwa ya watu wanaotaka 'kuishi kwa amani mtandaoni' wameunga mkono japo kwa maneno haja ya kukemea unyanyasaji mtandaoni. Lakini kama ilivyojitokeza leo jioni ambapo nimekuwa mhanga wa ushiriki katika harakati hizo, bado kuna wenzetu wanadhani wana hatimiliki ya kuwabughudhi watu mtandaoni watakavyo. Inabidi tuseme enough is enough. Kwa vile haijawahi kutokea huko nyumbani kwa mtu kuingia matatizoni kutokana na alichoandika mtandaoni, watu wengi tu wanaendelea kudhani kuwa akiwa mbele ya keyboard ya kompyuta yake ana uhuru wa kunyanyasa, kudhalilisha, kutukana na kufanya matendo mengine ambayo kimsingi ni makosa kisheria.

Ukweli ni kwamba tukiacha 'njia za asili' za kudhibiti 'wakorofi' kwenye mitandao ya kijamii, yaani aidha kuwa-mute, kuwa-unfollow au kuwa-block, kuna njia za ufanisi zaidi kama vile za kisheria alimradi kuna ushahidi wa kutosha.

Hatimaye nimefikia uamuzi wa kuchukua hatua za vitendo dhidi ya unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying). Sifanyi hivi kwa minajili ya kuingia kwenye vitabu vya historia kama Mtanzania wa kwanza kupambana na cyberbullies kwa vitendo bali ninafanya huduma kwa umma. Huhitaji kuwa kiongozi ili kuitumikia jamii. Na sihitaji madaraka ili niweze kupambana na tabia hii isiyofaa. Hakuna miujiza itakayowalazimisha wanyanyasaji wa mtandaoni kuacha tabia hiyo. Kitu pekee ni pale wanapofunzwa madhara ya vitendo vya aina hiyo.

Japo ningependa kuwa sehemu ya kundi linalopambana na suala hili, hadi sasa hakuna dalili zozote za uwepo wa mkusanyiko wa kukabiliana na tatizo hili ambalo kwa hakika linawasumbua wengi. Lakini tukisema tusubiri mpaka watu wajipange na kuunda kikundi, wenzetu wengi zaidi watazidi kuwa wahanga wa unyanyasaji huo wa mtandaoni.

Natambua ugumu wa mapambano haya lakini kila mapambano ni magumu. Natambua kutakuwa na lawama na kukatishana tamaa lakini liwalo na liwe lazima mtu flani awe mfano kwa wenzie kwamba cyberbullying is not just wrong but also a criminal offence.

Lengo la makala hii sio kumtisha wala kumzuwia mtu kunituhumu kuwa nami ni cyberbully. Ninaheshimu uhuru wa kujieleza alimradi hauvuki mpaka.Na kitu ambacho kamwe siwezi kukivumilia ni uvunjifu wa sheria dhidi yangu.

Ni matumaini yangu kuwa kama inavyofundisha Biblia Takatifu kuwa 'ukipiga mchungaji kondoo watasambaa,' kumwajibisha mmoja wa wanaodhani mitandao ya kijamii ni fursa ya kuwanyima wenzao amani kutapeleka ujumbe kwa wengine wanaoamini hivyo pia. Mafundisho ya Kiislam yanatueleza kwamba "ukiona jambo baya basi aidha lichukie, au likemee au liondoe." Nimeshachukia unyanyasaji mtandaoni vya kutosha, nimeukemea vya kutosha, na sasa ni wakati wa kuuondosha kwa vitendo. Haitokuwa rahisi lakini nina hakika nitafanikiwa. Inshallah!

Chahali: #StopCyberbullying: Kutoka kulalamika tu dhidi ya unyanyasaji mtandaoni hadi kuchukua hatua thabiti