Diaspora idhihirishe itakavyoisaidia Tanzania

TUMESHAZOEA maneno ya wanasiasa wanapopiga kampeni za kutafuta kuchaguliwa na wananchi. Wengi wao wanakuja na ahadi kemkem kama njia ya kutaka kuwavutia watu kuwa wao ndio wanafaa katika nafasi hiyo ya uongozi inayogombewa.

Si ajabu katika kipindi hiki kusikia ahadi za kila aina zikiwemo na zile ambazo kwa hakika kila mmoja anajua kuwa hazitekelezeki. Si ajabu kusikia mgombea akiahidi kujenga daraja katika kijiji ambacho hakina mto.

Kwa ujumla, wagombea hao wanaweza kutoa ahadi ambazo ni za kufikirika zaidi. Wengine wanalazimika kufanya hivi kama njia ya kukabiliana na ushindani kutoka kwa wagombea wengine. Wanaamini kuwa wasipotoa ahadi zinazozidi zile zilizotolewa na mgombea mwingine, wapiga kura wanaweza kuvutika zaidi na yule mgombea mwingine.

Tabia hii ya kutoa ahadi bila kuangalia uhalisia wa mambo katika eneo husika kwa upande mwingine inachochewa na ujinga wa wananchi wenyewe. Wengi wa wananchi wanaonekana kuweka mbele ahadi za

mgombea kama kipimo kizuri cha nani miongoni mwa wagombea walio mbele yao anafaa kuwa kiongozi wao.

Wananchi wengi hawatumii vigezo vinavyofaa kupima uwezo wa kiongozi. Ndio maana mara nyingine inakuwa ni rahisi sana kuwarubuni wapiga kura kwa vitu vinavyodumu kwa muda mfupi kama nguo na chakula.

Kwa bahati mbaya sana masuala haya ya kupeana ahadi yanaanza kuingia kwenye sekta nyingine. Kwa muda mrefu sana kumekuwa na kampeni za kutaka kuruhusiwa kwa utaratibu wa uraia pacha. Yaani mtu mmoja anakuwa na uraia wa Tanzania na uraia wa nchi nyingine ughaibuni ambako mara nyingi ndiko anakoishi.

Kwa kiasi kikubwa madai haya yanatolewa na watanzania ambao wanaishi nje ya nchi. Kwa kiasi kikubwa, kilichofanywa na watanzania hawa ili kuwaaminisha wengine kuwa ombi lao ni la maana ni ahadi za maneno matupu. Bado hawajafanya chochote kwa vitendo cha kutuhakikishia kuwa yale maneno wanayoyatoa yana ukweli ndani yake.

Mara nyingi watu hawa wanatueleza kuwa wakifanikiwa kuwa na uraia wa nchi mbili watakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuja kuwekeza nyumbani. Kwamba kinachowazuia hivi sasa kuwekeza na kuleta faida za kiuchumi ni kutokuwa na uraia wa ile nchi nyingine ambako wanaishi.

Lakini sote tunafahamu kuwa hata katika mfumo wa sasa, bado watanzania hao wanaoishi nje ya nchi wanayo nafasi ya kuwekeza, hata kwa kiwango kidogo sana, hapa nchini. Lakini wengi hawajaitumia fursa hiyo! Wanasubiri mpaka wawe na uraia wa nchi mbili ndipo waanze kuwekeza.

Lakini jambo la kujiuliza hapa ni kuwa kama wanashindwa kufanya kile ambacho kinawezekana kufanywa hivi sasa, yaani kuwekeza hata kwa kiwango kidogo, wataweza kweli kuwekeza pale watakapopewa uhuru wanaolilia?

Rais Jakaya Kikwete amewaeleza majuzi kwenye mkutano wao kuwa linapozungumzwa suala la uwekezaji, kwanza si lazima uwe ni wa kiwango cha miradi mikubwa mikubwa.

Aliwaeleza kuwa uwekezaji unaweza kuwa hata mdogo sana kwa sababu kulingana na hali ya nchi hata huo uwekezaji mdogo unaleta athari chanya kubwa kwa nchi.

Lakini kwa miaka yote hiyo tumeshindwa kuona hilo likitokea. Hata katika suala la utumaji fedha nyumbani, Tanzania ni miongoini mwa nchi ambazo watu wake walio nje ya nchi hutuma fedha kidogo sana nyumbani tofauti na nchi nyingine kama vile Kenya ambako mapato kutoka kwa watu walioko Diaspora ni makubwa sana.

Lakini jambo jingine ambalo Rais Kikwete aliwaeleza ni kuwa kuwekeza si lazima kufanywe na watanzania walioko nje moja kwa moja. Watanzania hao wanaweza kuwashawishi watu wengi wa nje kuja kuwekeza nchini.

Lakini hatujaona hili nalo likifanyika kwa nguvu. Masuala haya yote mawili hayahitaji uraia wa nchi mbili. Ni fursa zilizo wazi kwa mtanzania yeyote aliye nje ya nchi. Kama kweli hawa wanaodai uraia pacha wana dhamira ya dhati kutaka kuisaidia nchi, kwa nini hawajazitumia fursa hizi kama njiia ya kuonyesha dhamira yao ili tuwaamini?

Lakini kwa upande mwingine, hakuna uwekezaji mkubwa ambao nchi inaufanya kwa watu wake kama elimu. Kuna sehemu ya watu hawa walio nje ya nchi ambao walipelekwa, au walikwenda kwa juhudi zao, kutafuta elimu zaidi huko ughaibuni.

Lakini baada ya kufanikiwa kuipata elimu hiyo wakaamua kubakia huko nje na kuanza kudai wapatiwe uraia pacha ili waisaidie nchi yao.

Wanadai hivyo wakati elimu waliyonayo wanaweza kuja kuitumia hapa nchini kwa manufaa yao wenyewe, ndugu zao na taifa kwa jumla. Lakini wao hawalioni hilo na badala yake wanachokiona ni kupata uraia wa nchi mbili kama daraja la wao kuwa na uwezo zaidi wa kuisiaida nchi. Kama nchi ilishawasaidia wao kupata elimu nje ya nchi, hivi wanafikiria kuisaidiaje nchi kutokana na kile ilichowasaidia kukipata?

Nadhani kuna haja ya watanzania walio nje ya nchi, ambao wanadai uraia wa nchi mbili, kutuonyesha kwa vitendo hivi sasa hiyo dhamira yao ya kuisaidia nchi. Kama hawawezi kuzitumia fursa ndogo ndogo zilizopo hivi sasa, inatia wasi wasi sana kama kweli wataweza kuitumia ipasavyo fursa hiyo kubwa wanayoiomba.

Lakini wanaodai uraia pacha wanapaswa kufahamu kuwa suala la uraia ni moja kati ya masuala nyeti ambayo maamuzi yake yanapaswa kufikiwa baada ya tafakuri nya kina na ya makini. Si suala la kuliamua kwa haraka haraka kwa sababu pamoja na kuwa manufaa yake ya moja kwa moja ni kwa watu wachache, lakini madhara yake yanaweza kuwa kwa watu wengi wakiwamo ambao wala hawajui ni nini maana ya uraia pacha.

Imeandikwa na Bwana Mdogo via gazeti la Tanzania Daima