Akizungumza jana (juzi) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya barabara katika Manispaa hiyo, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli alisema kwa mujibu wa vifungu vya sheria ya ardhi na barabara inasema iwapo barabara ikimfuata mtu eneo alipo lazima mtu huyo apewe fidia, na mtu atakayeifuata barabara hataweza kupewa fidia yoyote.
Kwa mujibu wa Dkt. Magufuli, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiidai serikali tayari
wamelipwa kulingana na madai yao, na kuwa Serikali haipo kwa ajili ya kuonea watu na watu wasiionee serikali.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo Serikali imekusudia kujenga barabara hiyo kwa urefu wa kilometa 4, meta 7 za upana pamoja na kutenga eneo lenye ukubwa wa meta 4 kwa ajili ya waenda kwa miguu.
”Ujenzi ulianza mwaka 2013 mwezi wa 8, na kiasi cha Tsh. bilioni 6.4 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha mradi huu na mradi huu wenye awamu mbili unatarajia kukamilika mwaka 2016 na pia kiasi cha Tsh bilioni 1.6 zinatumika katika ajili ya utanuzi wa barabara ya Kibamba yenye km 1.4” alisema Mfugale.