Hallo? Mkude Simba….ANAWEZA kuwa msanii pekee hapa Tanzania ambaye ameweza kujiumba upya kisanii. Miaka miwili iliyopita, kila mtu alikuwa akimfahamu kwa jina la kisanii la Kitale.

Kitale, kisanii, alikuwa kijana mtumiaji wa dawa za kulevya. Mwizi, mdokozi na mtu asiye na mbele wala nyuma katika maisha yake. Kwa lugha ya Kiswahili cha kisasa, Kitale alikuwa teja.

Lakini, mwaka huu, Kitale amebadilika. Sasa anaitwa Mkude Simba. Mkude, kisanii, ni mchekeshaji ambaye anakuvunja mbavu kwa majibu yake ya kwenye simu.

Kwa sasa, kila mtu akisikia Haloo, mimi Mkude Simba, anajua kwamba kichekesho kinafuata sasa.

Kama spidi ya kukubalika kwa Mkude Simba itaendelea kuwa hii iliyopo sasa, miaka michache ijayo anaweza kabisa kumpoteza sokoni Kitale.

Na hili si jambo la kawaida. Lakini Mussa Kitale aka Kitale aka Mkude Simba aka Baba Bwakila ameweza kufanya.

Raia Mwema limekutana na Mkude Simba wiki hii na haya ndiyo yalikuwa mahojiano yetu.

Swali: Nani alikushawishi kuingia kwenye sanaa?

Kitale: Kabla sijaanza kuigiza nilikuwa naangalia michezo ya kuigiza ya Kundi la Kaole. Katika maigizo hayo nilikuwa nikivutiwa sana na waigizaji Adam Melele ‘Swebe’ na Abdul Ahmed ‘Ben’ na ndio walionishawishi kuingia kwenye sanaa. Kundi langu la kwanza lilikuwa Kaole na nilikuwa naigiza kawaida si vichekesho lakini sikuwa maarufu kipindi hicho.

Nilikuja kujulikana baada ya kujiunga na kundi la Fukuto linaloongozwa na Tuesday Kihangala ‘Mr Chuzi’ kwenye igizo la Jumba la Dhahabu.

Swali: Ilikuwaje ukaanza kuigiza kama teja?

Kitale: Wakati naangalia maigizo ya Kaole, Benny na Swebe walikuwa wanaigiza nafasi kama hizo za vijana wa kihuni lakini nikaona kuna fursa ya kuongeza zaidi ili kurekebisha nilichokiona. Nikajifunza maisha ya mateja kwa sababu maeneo niliyokuwa naishi ya Mwananyamala ndiko mateja wamejaa.

Sikuwa nakaa nao kwa kutumia hizo dawa za kulevya bali nilijenga nao urafiki nikawa najua maisha yao na vitu wanavyofanya wakiwa wamelewa zaidi hivyo ikawa rahisi kwangu kuigiza kama teja na kufikisha ujumbe kwa jamii wa maisha hayo.

Swali: Hivi sasa umeingia kwenye sanaa ya muziki, Je ni aina gani ya muziki unafanya na una nyimbo na albamu ngapi?

Kitale: Muziki niimbao ni aina ya katuni hauna mtindo mmoja. Ni mchanganyiko na vichekesho ndani yake. Nina nyimbo zaidi ya 15 nimetunga lakini nimetambulisha moja inayoitwa “Hili Dude Noma” sina mpango wa kuuza albamu kutokana na soko la sasa alihitaji albamu sana.

Swali: Tofauti ya Mkude Simba na Kitale ni nini?

Kitale: Mkude Simba ni brand inayomtambulisha Kitale katika njia nyingine ambayo inafanya vitu vingi ikiwemo matangazo. Ukimzungumzia Kitale ni kama anavyofahamika kawaida muigizaji wa siku zote. Mkude Simba imekubalika sana sikutegemea na washukuru mashabiki wangu nitatumia nafasi hii kutengeza vitu vyenye ubora kama walivyonikubali.

Swali: Wewe na marehemu Hussein Mkiety ‘ Sharo Milionea’ mlikuwa mkiigiza sehemu moja mnaendana sana , Je kuna msanii umeona anaweza kusiba pengo lake hadi sasa?

Kitale: Sijona mwigizaji anayeweza kuziba nafasi ya Sharo Milionea hadi hivi sasa. Sharo ni msanii aliyekuwa na kipaji cha pekee na ndio maana alipoletwa na Snura kujiunga na kundi la Fukuto walikuwa wanataka kumkataa mimi nikatilia mkazo abaki kwa kuwa kuna kitu nilikiona kwake. Ndio mwanzo wa mimi na yeye kuwa marafiki hadi watu wakajua ni ndugu tumetokea wote Tanga wakati mimi ni Mluguru.

Swali: Ukiwa na familia yako wewe ni mtu wa aina gani?

Kitale: Nakuwa kama baba wa kawaida na nafanya majukumu yote ninayotakiwa kuifanyia familia. Pia nikipumzika tunapenda kuangalia filamu za Bongo hasa kazi nilizoshiriki.

Swali: Mwanao anakuchukuliaje anapokuona katika hali hiyo ya uteja ukiwa unaigiza?

Kitale: Mwanangu anafurahi sana na tunacheka pamoja na kucheza kwa kuwa nimemuelewesha na anajua ninachokifanya ni kazi. Pia matangazo ya Mkude Simba yamemfanya ajione ni mtoto wa pekee kwa kuwa wenzake siku hizi shuleni na mtaani wanamuita Bwakila mtoto wa Mkude Simba.

Swali: Umewahi kupata matatizo yoyote ya kiusalama kutokana na unayoigiza na umewahi kufikishwa kituo cha polisi?

Kitale: Ndio Polisi waliwahi kunifuatilia wakihisi mimi nauza na kutumia dawa za kulevya lakini si kitu cha kweli na wenyewe wamefuatilia wakagundua si kweli naigiza kwa ajili ya kuelimisha watu.

Ni kitu ambacho kilinishangaza kuona watu wanakosa kazi za kufanya wananifuatilia wakiwa wanajua kabisa mimi naigiza tu. Hawakunifikisha kituoni kwa kuwa nilipojua wamekuja nyumbani wananitafuta nilifikia nyumbani kwa rafiki yangu nikawaita watu wangu walioenda kuongea nao.

Swali: Unatumia kilevi chochote?

Kitale: Sinywi pombe wala kuvuta bangi ila sigara navuta kutokana na ninavyoigiza kama mhuni natakiwa nitumie kitu kinachoenda na bangi. Chakula changu kikubwa ni ugali dagaa, matembele na mlenda. Hivi sasa nafungua kinywa na matunda kinywaji natumia maji kwa kuwa nataka nipunguze mwili nimenenepa sana.

Swali: Kitu gani unatamani kukifanya unashindwa kutokana na kazi yako?

Kitale: Natamani niache gari nitembee mitaani kwa mguu lakini nashindwa kwa kuwa mashabiki wangu ni wengi wakubwa kwa wadogo hivyo naweza kufuatwa na mtaa mzima nikipita. Kuepusha hali hiyo natumia gari binafsi kila mahali ninapoenda.

Swali: Kwa wale vijana wanaotumia dawa za kulevya kweli ukikutana nao huwa wanakuchuliaje?

Kitale: Wanajua ninachokifanya na tumekuwa marafiki kwani nakaa nao na tunaongea mambo mbalimbali yanayohusu maisha kama wataona wanachokifanya ni kibaya wataacha wenyewe.

Swali: Kuna vijana wengi wanakaa sana vijiweni bila kazi yoyote ushauri wako nini?

Kitale: Mimi nasema waendelee kukaa waibe, wavute bangi na kufanya ufuska wowote lakini watambue fainali uzeeni kwa kuwa kuna wazee wengi tunawaona hawana muelekeo na sababu hawakutumia ujana wao kwa malengo.

Hata vitabu vya dini vinasema kijana akifikia mahali mwanaume anatakiwa awe na mke na mwanamke aolewe ili kila mmoja awe na majukumu na kufanya kazi kwa bidii ili aweze kutunza familia yake lakini wanapuuza hivyo vitu.

Swali: Kama ungekuwa kiongozi wa juu serikalini au ukapewa madaraka hivi sasa, kitu gani kikubwa ungebadilisha unachokiona ni kero katika jamii?

Kitale: Kwanza kabisa ningejenga barabara za juu kama wenzetu walivyofanya kupunguza foleni. Barabara tulizonazo na watu wanamiki magari 20 familia moja itafika mahali mtu unakaa kwenye foleni siku nzima bila kufanya kitu chochote kimaendele.