Ikulu yalaumiwa kuwa pango la mbwa waliokula watu, mifugo


Na Nickson Mahundi, Ludewa.

Utata umeendelea kugubika kwa wananchi wa wilaya ya Ludewa kuhusiana na mmiliki wa mbwa ambao walimuua mtoto Ibrahim Faraja Chipungahelo, Bw. Bosco Thobias Lingalangala uhalali wa kuyanunua baadhi ya majengo ya Ikulu ndogo ya wilaya ya Ludewa na kugeuza sehemu ya kufugia mbwa ambao ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Hali hiyo ya sintofahamu imeendelea kuwashangaza wananchi hao wenye shauku ya kuhoji kwa
viongozi mbalimbali wa kitaifa watakatembelea wilaya hiyo kuanzia sasa kutokana na miliki huyo kumiliki majengo hayo ya Ikulu na kuendelea kuwatishia kwa bastola pindi wanapopita katika maeneo ya Ikulu hiyo.

Akiongea kwa jazba Bw. Kasbeth Mhagama wakati akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo la mtoto kuuawa na mbwa kisha kuliwa nyama alisema kuwa wananchi wameshangazwa na ujasiri wa mtu huyo kwa majibu yake ya kejeli kwa wafiwa.

Bw. Mhagama alisema tayari mbwa hao walikuwa wameshawala mbuzi zaidi ya 57 lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa katika hilo na mmiliki huyo amekuwa na nguvu kubwa ikiwemo ya kununua baadhi ya majengo ya Ikulu hali ambayo ni hatari sana kwa wananchi.

“tunashangazwa na hali hii inayoruhusu mwananchi wa kawaida kumiliki majengo ya Ikulu na kuwatisha watu na bastola kila wakati na tunajiuliza ni nani aliyeko ngazi ya juu Taifani anayempa kiburi hicho ambacho kinawafanya wananchi wa wilaya ya Ludewa wasiishi kwa amani,” alihoji Bw. Mhagama.