Ikulu yazungumzia taarifa kuwa Rais Kikwete alihoiwa na Obama kuhusu IPTL

MKURUGENZI wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu amekanusha madai yaliyotangazwa hivi karibuni kwamba, Rais Jakaya Kikwete amehojiwa na Rais wa Marekani, Barack Obama, kuhusu fedha za kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam jana kukanusha taarifa hizo zilizotolewa na moja ya gazeti la kila siku nchini, Rweyemamu alisema katika ziara ya Rais nchini Marekani hivi karibuni, hakukutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Obama.

“Rais pia alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na katika mikutano yote hiyo hakuna jambo lolote linalohusu IPTL lililojadiliwa wala kuulizwa.
“Huu ni uongo na ni habari ya kutungwa na habari kama hizi huandikwa kwa ajenda, sasa sijui hawa wenzetu waliandika kwa ajenda zipi” 

Alisema masuala yote yanayohusu kilichojiri katika mkutano huo na namna Tanzania ilivyonufaika katika sekta mbalimbali, yatabainishwa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.