Injili kutikisa Taifa katika Tamasha la Matumaini 2014; Azam FC, Mtibwa Sugara lazima kieleleweke 08.08.2014


UPAKO! Zikiwa zimesalia siku chache kuelekea katika Tamasha la Matumaini litakalofanyika katika Uwanja wa Taifa, Agosti 8, mwaka huu, pamoja na burudani mbalimbali, waimbaji wa muziki wa Injili watakuwepo kulipamba tamasha hilo.

Akizungumza na Mikito Nusunusu, mratibu wa tamasha hilo, Luqman Maloto alisema kila kitu kimekwenda kwenye mstari na kinachosubiriwa ni muda ufike, Watanzania wajumuike kwa pamoja uwanjani kushuhudia burudani zisizo na mfano.

Kwenye muziki wa Injili, Maloto alisema mkongwe wa nyimbo za Injili, Upendo Nkone ataliongoza
jukwaa kwa kuporomosha nyimbo kama Haleluya Usifiwe, Mwambie Yesu, Unastahili Kuabudiwa, Usinipite Bwana na nyingine nyingi.

Kama hiyo haitoshi, watakuwepo Martha Mwaipaja anayetamba na wimbo wa Tusikate Tamaa na Ombi Langu, pia katika kundi hilo wapo Ambwene Mwasongwe, Angela na Paul Clement.
Katika kuleta raha zaidi, Maloto alisema mgeni rasmi safari hii atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

“Dk. Bilal ndiye atakayepuliza kipyenga kuanza kwa mechi kati ya Wabunge Mashabiki wa Simba dhidi ya wenzao wa Yanga.”

Mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo, Martha Mwaipaja.

Mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo,Ambwene Mwasongwe.

Kwa upande wa Wabunge wa Yanga imefanya usajili wa nguvu kwa kumchukuwa, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Jakaya Kikwete wakati Simba wamefanikiwa kumsajili, Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa
Pia viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwemo mawaziri na mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hilo na kuandika historia kwa pamoja.

Maloto amesema kutakuwa na mpambano mkali kati ya bondia anayeshikilia mkanda wa UBO, Thomas Mashali dhidi ya Mada Maugo ambaye hajawahi kumpiga mwenzake huyo katika pambano lao lilofanyika mara ya mwisho.

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kumuona mkali wa muziki wa dansi, Khalid Chokoraa akizichapa dhidi ya Said Memba huku mastaa wa Bongo Movie Jacob Steven ‘JB’ akizitwanga na Cloud 112.”

Ndondi nyingine za kukata na shoka ni pale Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba atakapozichapa ulingoni na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala.
Mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo, Upendo Nkone.

Maloto aliongeza kuwa kutakuwa na mechi kali za mpira wa miguu ambapo Azam FC itaumana vikali na Mtibwa Sugar.Kama hiyo haitoshi, Bongo Movie watakipiga na Bongo Fleva. Akasema burudani haitaishia hapo, kwani mastaa kibao wa Bongo Fleva watakuwepo kupiga shoo baab’kubwa.

“Tutakuwa na mfalme wa Bongo Fleva, Ali Kiba. Mashabiki wategemee kusikia nyimbo zake zote kali sambamba na hizi mpya za Kimasomaso na Mwana.”Mastaa wengine watakaolipamba jukwaa siku hiyo ni pamoja na Madee, Meninah, Scorpion Girls, R.O.M.A, Nyandu Tozi, Navy Kenzo, P-Plan, Shilole, Juma Nature na kundi zima la TMK Wanaume Halisi.

Tamasha la Usiku wa Matumaini limedhaminiwa na Vodacom, Pepsi, PSI, Benki ya Posta, GEPF, Azam TV, E.FM (93.7), Gazeti la Championi, Times FM (100.5), SYSCORP na Clouds FM/TV.