Kauli ya CCM kuhusu yatokanayo na mdahalo wa Katiba Mpya ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika Mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, uliofanyika tarehe 04/08/2014 mjini Dar es salaam, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mzee Joseph Sinde Warioba na baadhi ya wajumbe wenzake pamoja na mambo mengine, walikitupia lawama nyingi Chama Cha Mapinduzi na Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete kwa hisia nyepesi, dhaifu na za kutunga. Mara kadhaa na hata katika mdahalo uliopita, baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Warioba wamekuwa wakitumia muda mwingi kujaribu kupotosha umma na kuwashambulia wote wenye mitazamo tofauti na ya kwao. Inaelekea baadhi ya wajumbe wa Tume ya Warioba wameufanya mchakato wa Katiba kuwa mali yao na kufanya kila juhudi za kujitengenezea hati miliki ya Katiba. Katika mazungumzo yake Mzee Warioba na wenzake wamekuwa wakitumia takwimu kutetea hoja ya serikali tatu.

Lakini hivi sasa wanahama na kusisitiza kuwa ni busara zao ndizo zilizopelekea kupendekeza muundo wa serikali tatu. Kimetokea nini? La kusikitisha zaidi ni kuwa; wamekuwa na msimamo mkali usiokubali kusikiliza na kutoa nafasi kwa mawazo yoyote yanayotofautiana na ya kwao. Badala yake
wanatumia juhudi kubwa kuwalazimisha Watanzania kukubaliana na maelezo yao hata kama yanaipeleka nchi pabaya.

Inaelekea Mzee Warioba na Tume yake wanaigeuza Rasimu kuwa MRADI BINAFSI ulioshikamanishwa na maisha yao, historia yao na heshima yao, tofauti kabisa na utamaduni wa tume nyingine za Katiba hapa nchini na duniani kote. Kudhihirisha ukweli huo, sasa wazee hao wameonesha hasira zao kwa kutumia kauli za dharau na kejeli kwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Aidha, wamekuwa wakitumia lugha kali na hata za vitisho kwa kutumia uzee kama walivyofanya mdahalo uliopita, kuwasema wale wote wenye mtazamo tofauti na wa kwao.

Rais Jakaya Kikwete siyo kiongozi pekee aliyetoa mawazo na ushauri katika mchakato wa mabadiliko ya katiba. Marais wote wa Tanzania walitoa maoni yao kwa njia ya ushauri kwa kutoa tahadhari na hata kwa kufafanua.

Rais ana wajibu kwa Taifa na kwa Watanzania. Ni kwa nini baadhi ya wajumbe hawa wafikirie kuwa wana haki na dhamana zaidi kuliko Rais wa nchi? Rais na Viongozi wengine katika nafasi zao na katika vikao vyao wanayo haki kama ile waliyokuwa nayo wajumbe wa Tume ya kutoa maoni yao ama ya kuunga mkono, ama kupingana, ama kuboresha na ama kupendekeza mabadiliko katika rasimu.

Haki hii inatolewa katika katiba yetu, imefafanuliwa katika sheria ya mchakato wa katiba na ipo wazi katika kanuni za Bunge maalum la Katiba. Chama Cha Mapinduzi kina haki na wajibu sawa na vyama vingine na asasi mbalimbali na watu binafsi katika kukosoa na kutoa maoni. Hakuna Chama cha siasa nchini kisichokuwa na mtazamo wake kwenye swala la katiba, inakuwaje dhambi kwa CCM kuwa na mtazamo wake na kuusema??! Hatuoni sababu za msingi za Tume kukishambulia na kukisakama Chama Cha Mapinduzi kwa kufanya uchambuzi na kutoa maoni yake kwa kuzingatia Katiba yake, sera zake na ilani yake.

Kwa mfano katika mdahalo wa juzi baadhi ya wajumbe hao walimshambulia Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Kikwete, walikishambulia Chama Cha Mapinduzi na wote wenye mawazo tofauti na ya kwao tena kwa kutumia maneno yasiyokuwa na staha wala ustaarabu.

Katika baadhi ya tuhuma zao wanadai Rais Kikwete na CCM waliingilia mchakato wa Katiba na kuuteka na hivyo kuuharibu. Tunajiuliza CCM na Rais Kikwete hawana haki ya kutoa maoni yao katika mchakato huu? Nani kalazimishwa kufuata mawazo yetu hata igeuzwe kuwa kutoa maoni yetu ni dhambi ya kustahili kejeli na matusi? Utaratibu huu wa baadhi ya wajumbe wa Tume ya Mzee Warioba kumkejeli Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa nchi yetu hauvumiliki hata kidogo.

Ikumbukwe kuwa Tume ilipewa uhuru wa kutosha bila kuingiliwa katika kazi yake ndio maana wakafikia walipofika. Hata pale waliposhauriana na Rais wakiwa na mawazo tofauti na yake, bado hakuwaingilia kwani alishawaahidi uhuru wa kutosha. Kwa maneno yao walitaka Rais awasukume kuchakachua ripoti yao? Uhuru na ushirikiano aliowapa leo unageuka fimbo ya kumsema na kumkejeli Rais? Hili halivumiliki.

CCM inapenda kuwakumbusha kuwa kazi ya tume ilishaisha, na kama ambavyo imekuwa kwa tume zingine nyingi nchini wanapaswa kutotumia mgongo wa tume kuendelea kuwapotosha Watanzania.

Kama ambavyo wadau wengine waliwavumilia wakati wanatimiza wajibu wao, wao pia wawe wavumilivu na waziachie awamu zilizobaki katika mchakato huu, zitimize wajibu wake kwa uhuru unaostahili. Ni muhimu kukumbuka katiba ni tunda la maridhiano, ili maridhiano yapatikane ni muhimu sana kuvumiliana na kuheshimu mawazo au maoni tofauti na yale ya kwako. Ni vizuri tusitumie mchakato huu kuelezea hasira zetu dhidi ya Rais kisa tu ni Mwenyekiti wa CCM.

Mchakato wa katiba utumike kama baraka na fursa ya kuijenga nchi yetu na sio kuibomoa kwa kupandikiza chuki na mifarakano. Utanzania wetu na Tanzania yetu ni ya thamani kuliko matamanio ya mioyo yetu na heshima zetu. Tuvitendee haki vizazi vyetu baada ya wazee wetu kufaidi matunda ya Muungano, vizazi vijavyo vina haki pia ya kuyakuta matunda haya. Tusiwanyime haki hiyo.

Imetolewa na:-

Nape Moses Nnuaye
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA 
ITIKADI NA UENEZI
07/08/2014