Mwandishi wa Habari Said Kubenea amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akiiomba mahakama itoe amri ya kusimamisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
Kubenea aliwasilisha ombi hilo juzi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala, akiomba Bunge hilo lisimamishwe hadi mahakama itakapotoa tafsiri sahihi ya bunge hilo kuhusu mamlaka iliyonayo na kama ni sahihi kwenda kinyume na rasimu.
Katika ombi hilo, Kubenea anaiomba mahakama itoe amri hiyo wakati wakisubiri uamuzi wa
mahakama kuhusu tafsiri sahihi kama bunge hilo linaweza kwenda kinyume na rasimu, pia tafsiri kuhusu mamlaka ya bunge hilo.
Aidha anaomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 25(1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi ambacho kinaeleza mamlaka ya Bunge hilo.
Ombi hilo lililowasilishwa chini ya hati ya dharura imeungwa mkono na hati ya kiapo ya Kubenea ambapo anaeleza, Desemba mosi mwaka 2011, Bunge la Tanzania lilipitisha mabadiliko ya Katiba na kuanza maandalizi ya kupata katiba mpya.
Anadai baada ya kuanza kwa Bunge hilo wajumbe walitofautiana kutokana na kuingizwa kwa hoja ambazo hazipo kwenye rasimu ndipo wajumbe wengine ambao ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakatoka bungeni kwa madai rasimu hiyo haiwezi kufanyiwa marekebisho kama wengune walivyokuwa wanadai. Ombi hilo limepewa namba 28 ya mwaka huu na linasubiri kupangiwa tarehe pamoja na majaji wa kusikiliza.
--
HabariLeo - Bunge Maalum mahakamani