THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameueleza mchakato wa kutafuta Katiba mpya nchini na changamoto zake kama barabara ndefu yenye kona.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa mchakato huo, kimsingi, unatakiwa kuongozwa na ukweli kuwa Katiba ni kuhusu wananchi wenyewe na maisha yao na wala siyo tu mchakato huo kuongozwa na idadi ya Serikali – mbili ama tatu.
Rais pia amesema kuwa ni dhahiri kuwa yapo mengi ambayo hayajakaa sawasawa katika mchakato mzima hasa kuhusu jinsi Katiba mpya itakavyolinda maisha ya wananchi na kusaidia kuboresha ustawi wao.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington wakati alipokutana, akazungumza na kujadili naWatanzania wanaoishi katika Marekani hasa kutoka maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya Virginia, Maryland, California na New York.
Akiwaeleza Watanzania kuhusu hali ilivyo nchini – kisiasa na kichumi – Rais Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa mchakato wa kutafuta Katiba mpya umekuwa unakabiliwa na changamoto kadhaa katika siku za karibuni.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao: “Najua kuwa mchakato wa Katiba umekuwa na changamoto katika siku za karibuni lakini kwangu mimi mchakato huo ni sawa na barabara ndefu ambayo haikosi kona. Kona zitakuwepo lakini mimi ni mtu ambaye anaishi kwa matumaini na ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendelea na hatimaye kufikia mwisho vizuri kama tunavyotarajia wote.”
Rais Kikwete ameongeza: “Aidha, naamini kuwa yapo mengi kuhusu Katiba ambayo hayajapata muda wa kutosha wa kuyajadili katika Bunge la Katiba. Kimsingi, Katiba ni Katiba ya wananchi, ni Katiba kuhusu maisha yao na ustawi wao. Hili jambo sijaona kama linaonekana sana katika mjadala wa Katiba.”
Ameongeza: “Mchakato wetu kwa muda mrefu umekuwa kuhusu idadi ya Serikali, ziwe mbili ama ziwe tatu. Kwangu mimi, idadi ya Serikali ni muhimu, lakini naamini kuwa Katiba iwe ni kuhusu maisha yenyewe ya wananchi na ustawi wao lakini mwelekeo mzima wa Mchakato huo usiwe kuhusu idadi ya Serikali tu.”
Rais Kikwete amesema kuwa anajua kuwa yamekuwepo maneno mengi kuhusu Katiba lakini akaongeza kuwa anaamini majawabu ya changamoto na matatizo ya sasa ya mchakato huo yatapatikana.
“Najua kuwa maneno yamekuwa mengi lakini siyo ndiyo demokrasia ya wazi inavyofanya kazi lakini sisi katika Serikali hatuna wasiwasi na hali hiyo. Ndiyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika nchi ambako demokrasia inafanya kazi. Yale mambo yanayotusumbua kwa sasa yanazungumzwa na vyama vyetu na naamini majawabu yatapatikana.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete amerudia kusema kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kisheria ambao utalinda mapato yatakayotokana na mauzo ya rasilimali ya gesi nchini kwa kizazi cha sasa cha Watanzania na vizazi vijavyo.
“Tutahakikisha kuwa tunaanzisha Mfuko Maalum kulinda fedha zitakazotokana na mauzo ya gesi. Raslimali hii pamoja na fedha ambazo zinatokana na rasilimali hiyo siyo mali ya kizazi chetu tu bali ni mali ya vizazi vijavyo vya Watanzania”.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti,2014