Kuhusu mfadhili mkuu wa ACT-Tanzania

TAARIFA YA ACT KWA UMMA
  1. Katika toleo lake la siku ya Jumatano ya tarehe 30 Julai 2014 Gazeti la Tanzania Daima limechapisha habari zilizodai kuwa mwanasiasa moja maarufu hapa nchini ndiye mfadhili mkuu wa Chama cha ACT-Tanzania.
  2. Kwa niaba ya uongozi wa ACT-Tanzania, na kwa nafasi yangu kama Mtunza Hazina na Mhasibu Mkuu wa ACT-Tanzania, napenda kuwataarifa wanachama na wapenzi wa chama na wananchi kwa ujumla kuwa taarifa hizi ni uzushi na uwongo wenye lengo la kuchafua taswira ya chama cha ACT-Tanzania. Napenda kuutaarifu umma kuwa moja ya misingi mikuu ya ACT-Tanzania ni uadilifu na uwazi. Kwa misingi hii, vyanzo vya mapato na matumizi ya ACT-Tanzania yapo wazi kwa mtanzania yeyote anayetaka kujua ukweli.
  3. Tangu chama kianzishwe mwezi Januari mwaka huu, kimeshapokea na kutumia jumla ya shilingi 74, 857,000/= (milioni sabini na nne laki nane na elfu hamsini na saba) zilizochangwa na wanachama, wapenzi na wananchi wasiopungua 50 wanaouunga mkono misingi ya chama hiki. Taarifa ya kwanza ya fedha ya chama iliwasilishwa katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya ACT-Tanzania katika mkutano uliofanyika Mjini Singida tarehe 25-26 Julai 2014. Kwa mtanzania yeyote ambaye angependa kuona orodha ya watu waliokichangia chama anakaribishwa kufika ofisi ya Makao Makuu iliyopo Ubungo National Housing mkabala na Hoteli ya Royal Njombe.
Pamoja na salamu za uzalendo za ACT-Tanzania
Peter Mwambuja, PGDA, CPA (T)
Mtunza Hazina na Mhasibu Mkuu wa ACT-Tanzania.

Imetolewa Jumatano 30 Julai 2014