Kuhusu mifumo 2 ya utungaji Katiba na Uwasilishaji wa nyongeza ya mapendekezo

Mtaalam wa sheri na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu ya Bunge hilo, Dkt. Francis Michael ametoa ufafanuzi kuhusu suala la utungaji wa Katiba ambalo hufanyika kwa mifumo miwili, na kuwataka wananchi wasipotoshwe na mfumo unaotumika.

Akizungumza katika kipindi cha Jambo kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) amesema:
  • Mfumo wa kwanza - Hutumia Tume kama ilivyokuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba yenye watu ambayo ilikuwa na kazi ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Katiba Mpya , baadaye Bunge Maalum la Katiba linapitia maoni ya Rasimu hiyo, ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2014 linaweza kubadilisha na kuongeza kwa ajili ya kuiboresha. “Katika mfumo huu lazima Bunge liwepo kwa ajili ya kuiboresha kabla ya kwenda kupigiwa kura na wananchi.” 
  • Mfumo wa pili - Hutumia Tume Maalum ya Wataalam, ambao wanawajibu wa kuandika Katiba na hakuna chombo chochote kitakachokuwa na wajibu wa kuibadilisha, bali itakwenda moja kwa moja kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura. “Wananchi wasichanganywe na mfumo unaotumika.” 

Uwasilishaji wa nyongeza ya mapendekezo 

Dkt. Michael amesema uwasilishaji wa nyongeza ya mapendekezo kutoka kwenye makundi mbalimbali hivi karibuni kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, yamepokelewa kwa mujibu wa sheria, kipengele cha 25 ambapo Bunge hilo lina nguvu kufanya marekebisho au kuongoza vifungu vingine pale linapoona inafaa.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Ridhiwani Kikwete alisema linafanyika kisheria hivyo mtu au kikundi kinaweza kuwasilisha mapendekezo ya nyongeza ambayo hufikishwa kwenye Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo, ambayo nayo hupeleka kwa Kamati 12 za Bunge hilo kwa ajili ya kuratibu mambo ya msingi na kuyachukua.

Pia, alisema hilo linaweza kufanyika wakati wa mjadala wa Bunge hilo, mjumbe anaweza kulishawishi Bunge hilo kwa kuwa sheria, kanuni na miongozo inaruhusu.