Maelezo ya Azimio la Kufanya Marekebisho ya Kanuni za Bunge la Katiba

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

BUNGE MAALUM


MAELEZO YA MWENYEKITI WA KAMATI YA KANUNI NA HAKI ZA BUNGE MAALUM, MHESHIMIWA PANDU AMEIR KIFICHO (MJ.),KWA AJILI YA KUWASILISHA AZIMIO LAKUFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA BUNGE MAALUM


(Kwa mujibu wa Kanuni ya 59(1) na 87(1) ya Kanuni za Bunge Maalum za mwaka 2014)
-----

Yatasomwa na:
Mhe. Pandu Ameir Kificho (MJ.)
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum.
DODOMA

5 Agosti, 2014
______________

1.0 UTANGULIZI

1.1 Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuwasilisha mbele ya Bunge Maalum, maelezo mafupi kabla ya kupitisha Azimio la Bunge Maalum kwa madhumuni ya kufanya mabadiliko ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014.

1.2 Aidha, napenda kukupongeza kwa dhati kabisa wewe binafsi na Makamu Mwenyekiti kwa namna mnavyoendelea kutuongoza katika Bunge hili Maalum katika vipindi vyote hadi kufikia wakati huu wa mjadala wa sura za Rasimu ya Katiba.

1.3 Vilevile, nikushukuru kwa niaba ya Wajumbe wenzangu wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum kwa kutuelekeza kuzijadili baadhi ya Kanuni za Bunge Maalum ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Bunge hili. Katikakutekeleza jukumu hilo, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Wajumbe wote wa Kamati yangu pamoja na Sekretariet ya Kamati kwa kufanya kazi uliyotupa kwa umakini mkubwa, na hatimaye kuandaa mapendekezo ya Marekebisho ya Kanuni hizi, ambayo kwa niaba ya Kamati, ninayawasilisha ili yajadiliwe na kama Bunge hili Maalum litaona inafaa, liyapitishe mabadiliko hayo ya Kanuni kama zilivyoelezwa katika waraka huu.

2.0 MCHAKATO WA KUFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA BUNGE MAALUM


2.1 Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni ya 59(1) ya Kanuni za Bunge Maalum, zinakupa wewe Mheshimiwa Mwenyekiti uwezo wa kupeleka mapendekezo ya kuzifanyia marekebisho au mabadiliko kanuni za Bunge Maalum katika Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum. Kwa mamlaka uliyopewa kwa mujibu wa kanuni ya 59(1), uliagiza Kamati ya Kanuni iangalie na kutoa mapendekezo kwenye maeneo yafuatayo:

(a) Siku na muda wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Bunge Maalum;
(b) Utaratibu wa kujadili Sura za Rasimu ya Katiba;
(c) Utaratibu wa kupiga kura kupitisha ibara za Rasimu ya Katiba;
(d) Usimamizi wa mahudhurio ya Wajumbe katika Vikao vya Bunge Maalum na Kamati zake;
(e) Uongozi wa Kamati ya Mashauriano; na
(f) Mwongozo wa uandishi wa Taarifa za Kamati.
Hivyo, uliiagiza Kamati yangu iziangalie upya Kanuni mbalimbali ili kuona haja ya kuzifanyia marekebisho. Baada ya kuzipitia Kanuni za Bunge maalum hususani katika maeneo tajwa hapo juu, Kamati imeona ipo haja ya kuzifanyia marekebisho kanuni zifuatazo: Kanuni ya 14, 15, 32, 32B, 33, 35, 36, 46, 47 54, 60, 62 na 65.

2.2 Baada ya mjadala kuhusu uzingatiaji wa kanuni zilizotajwa, Kamati yangu imeandaa Mapendekezo ya Marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalum kama inavyofafanuliwa katika jedwali la Marekebisho.

3.0 MAPENDEKEZO YA KUPITISHA AZIMIO LA KUFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA BUNGE MAALUM


3.1 Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo haya ya marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalum yanapendekezwa kufanywa ili kukidhi haja na kuleta tija katika uendeshaji bora wa Shughuli za Bunge Maalum. Kanuni zetu za Bunge Maalum zimeweka fursa hiyo ya kufanya marekebisho au mabadiliko ya kanuni hizo.
3.2 Mheshimiwa Mwenyekiti, Msingi wa kufanya marekebisho haya ya kanuni unatokana na sababu zifuatazo:

(a) Kanuni ya 14 inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kufuta fasili ya (4) ili kuondoa sharti la Bunge Maalum kukutana siku ya Jumamosi. Marekebisho haya yanalenga kuwapa Wajumbe muda wa kupumzika na kufanya tafiti na mashauriano juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Rasimu ya katiba ili kuboresha michango yao wakati wa Mjadala kwenye Kamati na ndani ya Bunge Maalum.

(b) Marekebisho ya Kanuni ya 15
Inapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kusimamia mahudhurio ya Wajumbe kwenye Bunge Maalum na Kamati zake. Kwa mujibu wa marekebisho hayo kila Mjumbe sasa atatakiwa kusaini yeye binafsi karatasi ya mahudhurio iliyoandaliwa na Katibu wa Bunge Maalum kama uthibitisho wa kuhudhuria kwake.

(c) Marekebisho ya Kanuni ya 32
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kanuni ya 32 mapendekezo ya marekebisho katika fasili ya kwanza (1) yanalenga kuondoa utaratibu uliokuwepo wa kila Kamati ya Bunge Maalum kujadili Rasimu ya Katiba kwa wakati mmoja kwa kuzingatia mgawanyo wa Sura angalau mbili za Rasimu ya Katiba zinazofanana. Hivyo, inapendekezwa kwamba kila Kamati ijadili Sura zote za Rasimu ya Katiba. Aidha, katika fasili ya pili (2), inapendekezwa muda wa kujadili Sura hizo ambapo Kamati zitajadili Sura za Rasimu ya Katiba kwa muda usiozidi siku kumi na tano(15). Utaratibu unaopendekezwa, utafanya Sura za Rasimu ya Katiba zilizobaki zijadiliwe kwa muda mfupi zaidi lakini kwa ufanisi mkubwa.

Vilevile, Kanuni hiyo inapendekezwa kufanyiwa marekebisho katika fasili ya (7) na ya (8) ili kuweka muda wa kuwasilisha mapendekezo ya Sura mpya kwa Katibu na pia kuipa mamlaka Kamati ya Uongozi baada ya kuridhika kuwa, mapendekezo yanayopendekezwa, yanakidhi kuwa Sura mpya au sehemu ya Sura ya Rasimu ya Katiba, kuelekeza mapendekezo hayo yajadiliwe na Kamati Namba Moja hadi Kumi na Mbili. Utaratibu uliopo kwenye Kanuni hivi sasa, mapendekezo hayo yanajadiliwa ndani ya Bunge Maalum na hivyo kutotoa fursa kwa Kamati kupitia mapendekezo hayo kwa kina zaidi.

Pia mapendekezo ya marekebisho katika fasili ya tisa (9) ya Kanuni hii yanalenga kuziwekea Kamati za Bunge Maalum muda wa kuandaa Taarifa zake kwa kuwa hivi sasa Kanuni hazielezi Kamati zitaandaa Taarifa zake kwa muda gani. Kwa mujibu wa marekebisho hayo, muda wa Kamati kuandaa Taarifa utakuwa ni siku tatu (3).

Aidha, inapendekezwa kuongeza fasili ya (10A) na (10B) kwa lengo la kuipa Kamati ya Uongozi mamlaka ya kutoa mwongozo wa namna ya kuandika Taarifa za Kamati, na pia kuweka masharti kwamba, endapo Taarifa ya Kamati itaandikwa kwa kukiuka mwongozo uliotolewa basi Taarifa hiyo haitakubalika.

(d) Marekebisho ya kanuni ya 32B
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni hii inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kuifuta na kuiandika upya kwa lengo la kuruhusu masharti ya Kanuni ya 46 na 46A yanayohusu Bunge Maalum juu mamlaka ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum kutoa adhabu yatumike pamoja na marekebisho husika katika kuendesha majadiliano kwenye Kamati.

(e) Marekebisho ya Kanuni ya 33
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni ya 33 inapendekezwa fasili ya (2) ifanyiwe marekebisho kwa kufuta maneno “dakika sitini” na badala yake kuweka maneno “dakika mia moja na ishirini” kwa lengo la kuongeza muda wa kuwasilisha Taarifa ya maoni ya Wajumbe walio wengi. Pia kufuta fasili ya (5), (6) na (7) na kuandikwa upya kwa lengo la kuongeza muda wa kuwasilisha maoni ya Wajumbe walio wachache kutoka dakika thelathini hadi “dakika sitini”, na pia kumpa Mwenyekiti mamlaka ya kuweka utaratibu utakaozingatiwa wakati wa mijadala ya Taarifa za Kamati. Aidha, inapendekezwa taarifa za Kamati kwa Sura zote za Rasimu ya Katiba zijadiliwe katika Bunge Maalum kwa muda usiozidi siku kumi na sita.

(f) Marekebisho ya Kanuni ya 35
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kanuni ya 35 inapendekezwa fasili ya (6) hadi (11) zifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuweka utaratibu wa namna ya kujadili na kupitisha masharti ya Sura za Rasimu ya Katiba pamoja na Sura mpya zitakazopendekezwa. Mapendekezo hayo yanaondoa utaratibu wa kujadili na kupitisha angalau Sura mbili za Rasimu ya Katiba kwa Kamati Namba Moja hadi Namba Kumi na Mbili, na badala yake inapendekezwa kujadili Sura zote za Rasimu ya Katiba kwa kila Kamati na hatimaye uamuzi kufanyika baada ya mjadala wa Sura zote kukamilika.

(g) Marekebisho ya Kanuni ya 36
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 36 inapendekezwa ifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuainisha utaratibu utakaotumika wakati wa kupigia kura ibara za Rasimu ya Katiba. Aidha, inapendekezwa upigaji kura kwa ibara za Sura zote za Rasimu ya Katiba ufanyike kwa muda usiozidi siku saba.

(h) Marekebisho ya Kanuni ya 46
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni ya 46 inapendekezwa kufanya marekebisho kwa kuongeza fasili mpya ya (2), (3) na ya (4) ambapo fasili mpya ya (2) inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kumpa mamlaka Mwenyekiti wa Bunge Maalum kutoa adhabu kwa mjumbe atakayekiuka masharti ya fasili ya (1). Mapendekezo haya yanakusudia kuimarisha nidhamu ndani ya Bunge Maalum. Aidha, inapendekezwa fasili nyingine za kanuni ya 46 kuanzia fasili ya pili mpaka tisa zifanywe kuwa kanuni mpya ya 46A.

(i) Marekebisho ya Kanuni ya 47
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni ya 47 inapendekezwa kubadili muda wa kuwasilisha Taarifa za Kamati pamoja na maoni ya Wajumbe walio wachache. Marekebisho hayo yanapendekeza Taarifa ya Kamati ya waliowengi iwasilishwe kwa muda usiozidi “dakika mia moja na ishirini” na maoni ya wajumbe walio wachache yawasilishwe kwa muda usiozidi “dakika sitini”.

(j) Marekebisho ya Kanuni ya 54
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 54 inafanyiwa marekebisho kwa kuongeza fasili mpya ya (6) kwa lengo la kuwatambua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum kuwa Wajumbe wa Kamati ya Mashauriano.

(k) Marekebisho Kanuni ya 60
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kanuni ya 60 inapendekezwa kufuta maneno “angalau mbili” katika aya ya (a), ili kuondoa dhana ya Kamati ya Uandishi kuandika upya ibara za Sura angalau mbili za Rasimu ya Katiba na badala yake Kamati hiyo itaandika upya ibara za Sura zote za Rasimu ya Katiba baada ya mjadala wa Sura zote kukamilika.

(l) Marekebisho ya kanuni ya 62
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya marekebisho katika Kanuni ya 62(2), inapendekezwa kufuta neno “mbili” ili kuondoa dhana ya Kamati za Bunge Maalum kujadili angalau Sura mbili za Rasimu ya Katiba na badala yake Kamati zitajadili Sura zote za Rasimu ya Katiba na Sura mpya zitakazojitokeza.

(m)Marekebisho ya Kanuni ya 65
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 65 inapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kusimamia mahudhurio ya wajumbe kwenye Kamati. Kwa mujibu wa marekebisho hayo, kila Mjumbe atatakiwa kusaini yeye binafsi karatasi ya mahudhurio iliyoandaliwa kwa ajili hiyo, na Katibu wa kila Kamati atawasilisha karatasi hizo kwa Katibu wa Bunge Maalum.

3.3 Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitishwa kwa Azimio hili la kufanya mabadiliko yaliyotajwa kama yalivyowekwa katika jedwali la marekebisho, kutaliwezesha Bunge hili kuwa na ufanisi zaidi kwa kuzingatia maudhui yanayopendekezwa na muda wa siku 60 zilizoongezwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

3.4 Mheshimiwa Mwenyekiti, Jedwali la marekebisho ya kanuni hizo limegawiwa kwa Wajumbe wa Bunge hili kwa ajili ya kujadili na hatimaye kama wataona inafaa, kupitisha marekebisho hayo.

3.5 Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa madhumuni ya kuliwezesha Bunge hili Maalum kupitisha Azimio la kufanya marekebisho hayo, naomba uniruhusu niwasilishe Azimio husika mbele ya Bunge lako kama ifuatavyo:

AZIMIO LA KUFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA BUNGE MAALUM ZA MWAKA 2014
______________


KWA KUWA, kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 87(1) ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014, Bunge hili limepewa mamlaka ya kufanya mabadiliko ya kanuni pale haja ya kufanya hivyo inapojitokeza kwa madhumuni ya kuleta ufanisi katika uendeshaji wa Shughuli za Bunge Maalum;
NA KWA KUWA, kwa kutumia mamlaka yake, Mwenyekiti wa Bunge Maalum ameleta mbele ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum kanuni zifuatazo:

(a) Orodha ya yaliyomo;
(b) Kanuni ya 14;
(c) Kanuni ya 15;
(d) Kanuni ya 32;
(e) Kanuni ya 32B;
(f) Kanuni ya 33;
(g) Kanuni ya 35;
(h) Kanuni ya 46;
(i) Kanuni ya 47;
(j) Kanuni ya 54;
(k) Kanuni ya 60;
(l) Kanuni ya 62; na
(m) Kanuni ya 65,

ili Kanuni hizo zijadiliwe na Kamati yangu na baadae kujadiliwa na Bunge Maalum na hatimaye kuzipitisha;

NA KWA KUWA, Kamati ya Kanuni imeshamaliza kazi ya kujadili kanuni hizo kwa mujibu wa maelekezo ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na kuleta 11mapendekezo ya marekebisho ya kanuni hizo kama ilivyoainishwa katika jedwali la marekebisho ya kanuni hizo;

NA KWA KUWA, Jedwali la marekebisho ya kanuni zilizojadiliwa na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum, limewasilishwa kwa Wajumbe wa Bunge Maalum kwa ajili ya kuridhiwa na Bunge Maalum;

NA KWA KUWA, mamlaka ya Bunge Maalum ya kufanya Mabadiliko au Marekebisho ya Kanuni kwa ajili ya uendeshaji bora wa shughuli za Bunge Maalum yanatakiwa yatekelezwe kwa Bunge Maalum kupitisha Azimio la Kufanya Marekebisho au Mabadiliko ya Kanuni za Bunge Maalum;

KWA HIYO BASI, Bunge Maalum linaazimia, linaridhia na kupitisha Marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalum, kama yalivyowasilishwa kwa Wajumbe wa Bunge Maalum, kama ambavyo Bunge Maalum litaona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

Azimio hili limewasilishwa na kupitishwa katika Bunge Maalum leo

Jumanne tarehe5 Agosti, 2014.