Mahakama yazuia uongozi wa muda NICOL

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeweka zuio la muda kwa uongozi wa muda wa Kampuni ya Uwekezaji ya Taifa (NICOL) kwa kuitaka kutojihusisha na biashara au shughuli yoyote ya kampuni hiyo hadi kesi ya msingi itakapokwisha.

Kesi ya msingi namba 91 ya mwaka 2014, iliyofunguliwa na wanahisa waanzilishi dhidi ya uongozi wa muda wa Kampuni ya NICOL).

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, John Utamwa, Julai 10, mwaka huu, baada ya kusikiliza maombi yenye namba 297 ya mwaka 2014 yaliyofunguliwa na waombaji; Philemon Mgaya, Thabita Siwale, Ibrahim Kaduma, Balozi Anthony Nyaki na Sylvester Barongo.

Uongozi wa muda wa NICOL) uliopo madarakani, ambao katika maombi hayo ni wajibu maombi, ni Dk. Gideon Kaunda, Elias Mwemezi, Joyce Nyanza, Ladislaus Salema, Elimsaidie Msuri, Emilian Busara na Adam Wamunza.

Wadai hao waliomba yasikilizwe upande mmoja kwa kile walichoeleza kuwa iwapo wangewapa notisi, wadaiwa wangesababisha hasara kwa kutoa fedha nyingi za NICOL) benki.

Katika maombi yao, waliiomba mahakama kuwazuia kuhamisha fedha kwa niaba ya NICOL), pia kurudisha Sh. bilioni 1.5 walizolipa katika akaunti, ambayo si ya NICOL, iliyopo Benki ya NMB na kwamba, walisababisha hasara kubwa kwa mali za kampuni hiyo.

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Utamwa ameamuru waombaji kuwafahamisha upande wa walalamikiwa uwapo wa shauri hilo.

via NIPASHE