Malumbano mengine Bunge la Katiba: Lisitishwe! Lisisitishwe!


Mwanasiasa mkongwe na mjumbe wa halmashauri kuu ya chama tawala CCM Dkt Raphael Chegeni, ameungana na wanasiasa na wanaharakati mbalimbali kutaka Bunge Maalumu la Katiba lisitishwe.

Dkt Chegeni ambaye amewahi kuwa mbunge wa Busega kwa tiketi ya CCM, amesema mchakato wa katiba ni wa maridhiano na kuonya kuwa mvutano unaoendelea sasa baina ya wajumbe wa bunge maalumu la katiba hautowasaidia watanzania kupata katiba mpya.

Kwa mujibu wa Chegeni, bunge maalumu la katiba linaloendelea mjini Dodoma halitaweza kupata
maridhiano pasipo kuwagawa Watanzania ambapo ameshauri bunge hilo kusimama kwanza kupisha chaguzi zijazo.

Wakati huo huo, vyuo vikuu vitano barani Afrika kikiwemo chuo kikuu cha Bagamoyo nchini Tanzania vimeunda mtandao wa pamoja utakaotoa mafunzo kwa wataalam wa serikalini ya namna ya kuingia mikataba kwa lengo la kulinda rasilimali za nchi husika zisiendelee kupotea kwa kisingizio cha uwekezaji.

Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha Bagamoyo Dkt. Mtalo Elifuraha amesema baadhi ya watalaam wanaoingia mikataba na nchi zilizoendelea wamekosa uelewa wa namna gani mikataba hiyo itainufaisha nchi au kuipa nchi husika hasara.

Dk. Elifuraha amesema kuwa wanampango wa kuanzisha shahada za jinsi ya uingiaji mikataba katika vyuo hivyo ili kuweza kuwapa mwanga zaidi watu wanaoingia mikataba katika nchi za Afrika.

via EAtv

Wabunge CCM wavutana

Mbunge wa Longido CCM), Michael Lekule Laizer, na mwenzake wa Viti Maalumu, Dk. Prudenciana Kikwembe, wamevutana kuhusu hoja ya kutaka Bunge Maalumu la Katiba lisimame kwanza hadi hapo mwafaka baina makundi yanayokinzana katika mchakato wa kutunga katiba mpya utakapopatikana.
Mvutano huo uliibuka wakati wa semina kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao ni wajumbe wa kamati tano za Bunge, juu ya umuhimu wa kusikiliza maoni ya wadau, iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo.
Katika maelezo yake, katika semina hiyo, Laizer alishauri Bunge hilo lisimame kwanza na kujikita katika kupata mwafaka baina ya makundi hayo.
Alisema kwa sasa Bunge hilo linaendelea, lakini kukiwa hakuna mwafaka na wengine wakiwa wamesusia mchakato huo na katiba kuonekana ni jambo la vurugu nchini kwa sasa.
“Wananchi ni wadau, kuna viongozi, vyama vya siasa, wataalamu, wasomi, tunaona pamoja na mchango wetu wataalamu na wanasiasa wameipotosha Tanzania, katiba imekuwa kama vurugu, utashi wa kisiasa hadi wananchi wanakosa kujua ukweli ni nini,” alisema.
Aliwaomba wawasilishaji mada kwenye semina hiyo, ambao ni kutoka Bunge la Jamhuri na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi za Kijamii, John Ulanga, kutoa maoni yao iwapo mchakato huo uko katika nafasi nzuri ya kuendelea.
”Kwa kutumia semina hii, kwa sababu hili jambo linaonekana kushindikana, kwa maoni yao wanasemaje, wananchi wanashindwa kuelewa kinachoendelea na msimamo ni upi?” alihoji Laizer.
Hata hivyo, ushauri huo ulipingwa na Dk.Kikwembe akisema kauli ya Laizer kusema wabunge wanashindwa kujadili rasimu ya katiba siyo kweli kwa kuwa wanaendelea kujadili.
”Hatujashindwa kujadili.Tunaendelea kuijadili.Na nina hakika tutafika mwisho. Suala la wenzetu (Ukawa) kutokuwapo ndani sidhani kama kutafanya sisi tushindwe kujadili kwa sababu tunajua ni maoni ya wananchi lazima tujadili,” alisema.
Hata hivyo, Laizer hakuridhika na kauli hiyo na kutaka kupewa nafasi ya kuzungumza zaidi, lakini Mwenyekiti wa semina hiyo, William Ngeleja, aliwasihi wajumbe kutoendelea kuzungumzia suala la katiba ndani ya semina hiyo ya wabunge na siyo wajumbe wa Bunge Maalum.
Alisema mada zinazohusiana na mchakato wa katiba zielekezwe kwenye Bunge Maalumu la Katiba na zipo taratibu za kupeleka maoni.
NUKUU:
“Wananchi ni wadau, kuna viongozi, vyama vya siasa, wataalamu, wasomi, tunaona pamoja na mchango wetu wataalamu na wanasiasa wameipotosha Tanzania, katiba imekuwa kama vurugu, utashi wa kisiasa hadi wananchi wanakosa kujua ukweli ni nini.”

via gazeti la Nipashe

JUKATA


JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA), limemuomba Rais Jakaya Kikwete asitishe Bunge Maalumu la Katiba, lakini pia limevionya vyama vya siasa nchini kuhusiana na vitisho vya kuwashughulikia wanachama wao kuhusiana na Bunge hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alisema kauli ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kwamba watawashughulikia wanachama wao, ambao ni wajumbe wa Bunge hilo si nzuri na kusisitiza kwa hali ilivyo sasa kuna haja Rais Kikwete asitishe Bunge Maalumu la Katiba.

"Yatosha tu kusema kwa sasa nchi imegawanyika vibaya kuhusu mchakato wa Katiba mpya na ulipofikia, haikuwa mshangao kushuhudia wajumbe watatu kutoka kundi la Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) wakitinga bungeni na kujiandikisha ili kuendelea na vikao vya Bunge, akiwemo Mwatuka (Clara) kutoka CUF.

"Wengine ni waheshimiwa Leticia Nyerere, John Shibuda na Said Arfi, wote kutoka Chadema na Chiku Abwao pia wa Chadema, ambaye baada ya kusoma upepo kuwa Ukawa wamesusia kiukwelikweli amekanusha na kwamba alikuwa na shughuli zake binafsi mjini Dodoma na wala hakufika kushiriki vikao vya Bunge.

"Vyama vyao vya CUF na Chadema vimeahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa kukiuka maamuzi ya vikao halali vya kichama, lakini jambo moja dhahiri ni kuwa hawa ni wahanga tu wa tatizo kubwa zaidi la mpasuko wa kitaifa," alisema Kibamba.

Alisisitiza kuwa suala la kuchukuliana hatua au kushughulikiana si zuri na halileti tatizo la ufumbuzi uliopo kwani hata Ukawa wenyewe wamegawanyika, CCM nao wamegawanyika na jambo la msingi ni kutafuta ufumbuzi wa kitaifa kwani kuna mpasuko mkubwa ndani ya Bunge Maalum la Katiba, kijamii na hakuna maridhiano ya kitaifa.

"Kuna wajumbe wamechelewa kufika Dodoma kwa kuwa wanaamini Bunge Maalumu halipaswi kuendelea kwa hali hii, aidha hata miongoni mwa wajumbe wa CCM kuna mpasuko wa waziwazi kati ya wanaoamini kuwa Bunge Maalumu halipaswi kuendelea kwa sasa kwa kuwa theluthi mbili haitaweza kufikia maridhiano yanayohitajika ili Katiba mpya iweze kuandikika," alisema.

Alisema kuna wajumbe zaidi ya wanne wa CCM wametoa sauti kuhusiana na Bunge hilo na kwamba wapo wengi na ni ishara kuwa CCM nako kuna mpasuko.

Alidai kuwa CCM imegawanyika katika makundi matatu kuhusiana na mchakato huo na kuyataja kuwa ni kundi la wanaoondoka madarakani, kundi la wasio na upande ambao wapo kimya na kundi la wanaotaka madaraka.

"Pia hata miongoni mwa wana Ukawa kumetokea mpasuko kati ya wale wanaoamini kuwa hakuna haja ya kushiriki Bunge Maalumu, ambalo hatima yake hakutazaliwa Katiba mpya na wale wanaoamini kuwa wana haki ya kimsingi ya kushiriki vikao Bunge Maalumu la Katiba na kupata posho zao kama wale wa CCM," alisema.

Pia alieleza kuwa kuna wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambao wameduwaa na hawajui la kufanya.

"Tunashauri kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili uanze tena Januari 2016 na kwamba ili kuokoa gharama za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, chaguzi hizi mbili zifanyike siku hiyo hiyo moja ya Uchaguzi Mkuu," alisema.

Pia Kibamba alieleza kitendo cha Ukawa kushindwa kurejea bungeni kinaunyima mchakato wa Katiba uhalali wa kisiasa na kisheria na kwamba upande wa wajumbe wa Zanzibar wanafanya kukosekana kwa theluthi mbili inayohitajika.

via Habari Leo

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA), limetoa tamko juu ya mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba na kusema kinachoendelea katika Bunge hilo ni matumizi mabaya ya fedha za umma hivyo wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kulisitisha hadi baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwani nchi imegawanyika vibaya kuhusu mchakato huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma kuhusu jukwaa lao, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Bw. Deus Kibamba, alisema kumekuwa na mabadiliko mengi ya sheria na kanuni ili kuongeza muda wa Bunge hilo kuendelea na vikao vyake hivyo kuongeza bajeti.

“Ikumbukwe kuwa, awamu ya kwanza ya Bunge hili imetumika fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo na maboresho ya ukumbi pamoja na posho za vikao kwa siku 67, sasa kumeibuka nyongeza nyingine ya muda wa Bunge maalumu kuwepo Dodoma.

“Kwa kutumia kanuni, Bunge Maalumu limefanikiwa kujiongezea muda wa kukaa Dodoma kwa siku 84 hadi 90, huku ni kupandisha fungu la matumizi ya Bunge ili kufikia sh. bilioni 30 ambazo ni pesa nyingi za walipa kodi,” alisema.

Alisema pesa ambazo zitatumika Dodoma kwa siku 90, zingetosha kutatua tatizo la maji katika Wilaya ya Kondoa na Kilindi kwa hesabu za mpango wa ufuatiliaji matumizi yaani PETS.

“Taarifa kutoka ndani ya Bunge hili, fedha zilizotumika kuanzia Agosti 5 hadi 9 mwaka huu ni takriban sh. bilioni 2.2 ambazo chanzo chake ni kubadilishwa kwa kanuni,” alisema Bw. Kibamba.

Aliongeza kuwa, kazi ya kurekebisha kanuni imezingatia mambo mawili kwanza kuwabana wajumbe waliotoka bungeni kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na wengine waliopo nje ya Bunge kwa kususia au sababu nyingine jambo ambalo linaweza kukwamisha mazungumzo yanayoendelea ili kuleta maridhiano.

“Majadala wa kanuni uliibua udikteta bungeni ukitaka itafutwe mbinu ya kupiga marufuku mijadala ya Katiba nje ya Bunge na kuwazuia wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wasizungumze chochote kuhusu Katiba badala yake waliache Bunge lifanye kazi yake.

“Mbaya zaidi, mjadala wa kanuni ulijikuta ukiingilia uhuru wa maoni na uhuru wa vyombo vya habari kwa kutaka vyombo vilivyokuwa vinara wa kurusha midahalo ya Katiba vishughulikiwe na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,” alisema.

Bw. Kibamba alisema, kubinywa kwa uhuru wa habari na maoni ya vyombo vya habari ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ibara ya 18 na 21(2), inayotoa haki kwa raia yeyote wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au Taifa.

Aliongeza kuwa, miongoni mwa wajumbe wanaotoka CCM nao wanampasuko kwani wapo wanaoamini Bunge hilo halipaswi kuendelea kwa kuwa theluthi mbili haitaweza kupatikana na joto la uchaguzi limepanda hivyo itakuwa ngumu kufikia maridhiano yanayohitajika ili katiba ipatikane.

“Wajumbe wa CCM wamekuwa wakitoa kauli hii bila kificho, hata miongoni mwa wana UKAWA, nako kuna mpasuko kati ya wanaoamini hakuna haja ya kushiriki Bunge Maalumu ambalo hatima yake hakutazaliwa Katiba Mpya na wanaoamini wana haki ya kushiriki vikao na kupata posho kama wajumbe wengine... wajumbe wanaotoka kundi la 201, wameduwaa na wahajui la kufanya,” alisema.

Alisema nje ya Bunge hilo pia kuna mpasuko uliowagawa Watanzania katika sekta mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyama, wafanyakazi, wakulima, wavuvi na vyombo vya habari hivyo yatosha kusema nchi imegawanyika vibaya kuhusu mchakato huo.

Bw. Kibamba alisema, tangu Bunge hilo lianze vikao vyake vya awamu ya pili, kumekuwa na tatizo la mahudhurio duni kwa wajumbe hasa kutoka kundi la 201 ambao hawajawahi kuripoti tangu kuteuliwa kwao.

“Imekuwa ngumu kwa Ofisi ya Bunge hili, kutoa orodha kamili ya wajumbe wote wanaounda Bunge Maalumu kwa ukamilifu wake na mahitaji ya kufanya hivyo... mbali ya wajumbe wa UKAWA kutorudi bungeni, bado mahudhurio ni mabaya.

“Wakati idadi ya wajumbe wa UKAWA ikifikia 200, mahudhurio ya wajumbe waliobaki zaidi ya 400 ambao ni wabunge na wawakilishi wa CCM pamoja na idadi kubwa ya wajumbe wa kundi la 201, imekuwa ikisuasua, Mawaziri, Manaibu Waziri na viongozi wengine wenye majukumu ya kiserikali, wanaongoza kwa kutoshiriki vikao vya Bunge hili,” alisema.

Alisema JUKATA wanaamini kuwa, mchakato wa kuandika Katiba Mpya si mradi wa mtu binafsi au kiongozi au chama chochote bali ni mradi endelevu wa wananchi hivyo Katiba ya kidemokrasia haiwezi kukamilika na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.

“Sisi tunashauri mchakato huu uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu 2015 ili uanze tena Januari 2016, tutakuwa tumeokoa gharama za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao tunashauri ufanyike siku moja na Uchaguzi Mkuu,” alisema Bw. Kibamba.

Aliongeza kuwa, mazungumzo kati ya vyama vya siasa hasa vilivyoko kwenye kundi la UKAWA na CCM, yafanyike haraka na kuhusisha wawakilishi wa kundi la 201 pamoja na wateule wachache kutoka taasisi za kidini, AZAKI na vyama vya wafanyakazi.

Alisema ipo haja ya kuirejesha iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kazi ya kulishauri Taifa na Bunge la Katiba kuhusu rasimu ya Katiba Mpya, masuala ya usanifu na maudhui ya Katiba kwa upana wake.


Pia yapo mahojiano ya Kibamba na gazeti la Raia Mwema "Jukata: Kwanini tunataka BMK lisitishwe"