Mcolombia akamatwa JNIA na cocaine alizozivaa nguoni

Suruali ya mtuhumiwa huyo ikiwa imezungushiwa Cocaine. (picha: Francis Dande)
Baadhi ya dawa alizokuwa amemeza mtuhumiwa huyo.

DAR ES SALAAM, Tanzania - KIKOSI cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kinamshikilia Andres Filipe Ballesteros Uribe (28) raia wa Colombia kwa tuhuma za kuingiza dawa hizo nchini kinyume cha sheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa kikosi hicho, Kamanda Godfrey Nzowa alisema mtuhumiwa huyo aliingia nchini saa nane usiku kwa ndege ya shirika la Ethiopian akitokea Adisi Ababa.

Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na cocaine iliyofungwa kwenye pakiti sita tofauti na kuiweka
sehemu za siri, kiunoni kama mkanda na nyingine tumboni.

Kamanda Nzowa alisema mtuhumiwa huyo mwenye pasi ya kusafiria namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014 nchini Colombia, alitoka Colombia kupitia Addis Ababa kuja Tanzania huku akibainisha kwamba hiyo ni njia mpya ya usafirishaji wa dawa hizo haramu.

“Hawa jamaa wanajaribu kubuni mbinu mpya kama huyu kijana alikuwa amefunga unga wa cocaine kama zilivyokuwa zikifungwa pipi na akazimeza… mpaka sasa ameshatoa pipi 13 kwa njia ya haja kubwa na anaendelea kutoa. …Sio rahisi kujua idadi ya mzigo aliokuwa nao mpaka atakapomaliza kuzitoa zote za tumboni ndiyo tunaweza kusema uzito wa dawa hizo na thamani yake,” alisema kamanda Nzowa.

Alisisitiza kwamba taarifa sasa wanazopeana kwenye mtandao wao unawezesha kukamatwa kwa watuhumiwa huku akibainisha kuwa lengo ni kudhibiti usafirishaji kwa njia yoyote.


Hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo yenye namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014 nchini Columbia. (picha: Francis Dande)
Akizungumza na Raia Tanzania, Nzowa alisema Felipe aliwasili kwa ndege ya Ethiopia Airlines akitokea kwao, Colombia, kupitia Ethiopia.

"Baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema, polisi wa JNIA na vijana wa kikosi changu, walimfuatilia hadi alipotua. Tulimweka chini ya ulinzi, katika mahojiano ndipo alipoonyesha dawa hizo.

"Kwa kadiri anavyoendelea kuzitoa tumboni, tunadhani zinaweza kuwa zaidi ya gramu 800. Tunamshikilia na mahojiano yanaendelea," alisema Nzowa.

Hata hivyo, mahojiano kati ya polisi na Felipe yamekumbwa na tatizo la lugha, kwani jeshi hilo halikuweza kupata mkalimani mara moja ambaye angesaidia kupata taarifa za kina za mtuhumiwa huyo na wengine wa kigeni wanaokamatwa uwanjani hapo na kubaini mtandao mzima.

"Itatuchukua muda sana kumuhoji kwa sababu anazungumza Kihispanyola. Tunafanya juhudi kupata wakalimani," alisema Nzowa.

Kamishna Msaidizi wa Polisi uwanjani hapo, Hamis Selemani alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, akisema, ameshaanza kutoa tumboni dawa alizozimeza.

Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa akionesha Cocaine zilizokuwa zimefichwa katika mkanda wa suruali aliyokuwa amevaa raia wa Colombia, Andres Filipe Ballesteros Uribe (28), mara baada ya kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (picha: Francis Dande)

Kamanda Nzowa alisema mafanikio yanaonekana kwa vile kuanzia Juni 24 mwaka huu hadi Agosti 10 hakuna mtu aliyekamatwa akiingiza huku akibainisha kwamba umadhubuti wa mtandao wao umefanikisha hilo.

“Asiyeamini kwamba tumefanikiwa atujaribu aone… naamini tunakokwenda dawa za kulevya hasa cocaine na heroine zitakuwa hazipiti wala kuingia Tanzania,” alisema na kuongeza kwamba wanadhibiti pia ulimaji wa bangi.

Kwa mujibu wa kamanda huyo lengo la mtandao wao ni kudhibiti sio kukamata wala kuteketeza.

via blogu ya Francis Dande na gazeti la Raia Tanzania