Mlemavu atumia mguu wake wa bandia kuuza dawa za kulevya

Kamishna Kova akiwa kashika moja ya dawa ya kulevya huku afande Alfred akiwa kashika mguu huo wa bandia anaotumia mlemavu.

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamshikilia Said Tidwa (36), mkazi wa Vijibweni, Temeke kwa tuhuma za kutumia mguu wake wa bandia kwa ajili ya kutunzia na kuuza dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda Maalum, Kamishna Suleiman Kova, alisema taarifa za kiintelijensia zilizopatikana kutoka kwa raia wema ziliwafikia makachero wa polisi kuwa Tidwa ambaye ni mlemavu wa mguu anajihusisha na biashara hiyo.

“Katika mtego maalum uliowekwa na askari wa upelelezi ndipo mlemavu huyo alikamatwa akiuza
dawa hizo kwa wateja wake baada ya kuzitoa alikozificha ambapo ni ndani ya mguu huo wa bandia” alisema Kova.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, mtuhumiwa huyo ana mguu wa bandia anaoutumia kuficha dawa hizo na kuziuza rejareja kwa wateja wake ambapo kila kete huuza sh. 1,000.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba mtuhumiwa huyo anatumia mbinu hiyo kwa muda mrefu kabla ya kukamatwa Agosti Mosi, mwaka huu,” alisema Kova na kuzitaja dawa alizokutwa nazo kuwa ni cocaine, heroine na wakati mwingine bangi.

“Natoa onyo kwa watu wenye ulemavu, wasitumie kigezo cha ulemavu kufanya uhalifu kwa makusudi kwani wanaharibia walemavu wengine ambao ni raia wema ambao sio rahisi kuwatilia shaka,” alisisitiza kamanda huyo.